Na WMJJWM- New York, Marekani
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amemwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa kipindi cha Kati cha Jukwaa la Kizazi chenye usawa (Mid Point) uliofanyika Septemba 17, 2023 jijini New York nchini Marekani.
Katika mkutano huo, Tanzania imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ahadi za nchi katika kuelekea Usawa wa Kijinsia ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kuwa kinara katika eneo la HAKI na USAWA wa KIUCHUMI.
Hadi sasa jitihada zilizofanywa na Tanzania katika kutekeleza ahadi hizo ni pamoja na kuundwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inayoweka kipaumbele eneo la usawa wa kijinsia na kuteuliwa kwa Kamati ya Taifa ya Ushauri yenye wajumbe 25 wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar inayoongozwa na Mhe. Angella Kairuki, Waziri wa Maliasili na Utalii.
Jitihada nyingine ni kuundwa kwa Programu ya Kizazi chenye Usawa Tanzania (Tanzania Generation Equality Programme - TGEP) inayotekelezwa na Wizara za kisekta kwa miaka mitano (5) Julai 2021/22 hadi Juni 2025/26 yenye mkakati wa kuleta mabadiliko ya ubora wa maisha ya wanawake na wasichana kwa kuimarisha Haki na Usawa wa Kiuchumi pasipo kuwaacha nyuma wanaume na wavulana kwa kuwajengea uelewa ili waweze kushiriki kwenye maendeleo ya Taifa.
Aidha, uteuzi wa maafisa viungo ngazi zote wanaosimamia utekelezaji wa haki na usawa wa kiuchumi kwenye maeneo yao na kuitambua Siku ya Wanawake Duniani sambamba na kushirikiana na Wadau kushughulikia changamoto za wanawake kama ilivyobainishwa katika Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 pamoja na Mpango wa Mkakati wake wa mwaka 2005, Maazimio ya Ulingo wa Beijing, Ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya Bara la Afrika 2063.
Waziri Dkt. Gwajima katika mkutano huo ameambatana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Riziki Pembe, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya utekelezaji wa Ahadi za nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa Mhe. Angellah Kairuki.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Abeda Rashid Abdullah na wataalamu mbalimbali.
Wakati huo huo ujumbe wa Tanzania umekutana na Mkurugenzi wa UN Women Dkt. Sima Bahous, ambaye ameipongeza Tanzania katika utekelezaji wa GEF na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo.