Na Mwandishi wetu- RUVUMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amezitaka Idara zinazohusika na ujenzi katika Halmashauri kuhakikisha zinajenga stendi za mabasi zenye ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa .
Waziri Jenista ametoa maagizo hayo wakati akizindua mradi wa ujenzi wa Stendi ya kisasa ya magari katika kijiji
cha Lundusi, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma unaotekelezwa na Ofisi ya Rais kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Aidha mradi huo unagharimu shilingi Milioni 482 huku ukitarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita tangu kuanza kwake.
Amesema ,"Katika awamu ya kipindi cha pili cha utekelezaji, TASAF imejikita katika masuala ya kuwezesha Kaya kutumia fursa za kukuza Uchumi na kuongeza kipato kwa kaya zenye walengwa pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya, Elimu na Maji Safi na Salama pamoja na miundo mbinu ya kukuza uchumi ngazi ya jamii,
“Wananchi wanasubiri Stendi bora ya kisasa na siyo stendi mbovu,idara zinazohusika na ujenzi kwenye Halmashauri sasa kumekucha na hatutarajii eneo la manunuzi ya ujenzi yakawa ni kichaka cha upotevu wa fedha kutoka Ofisi ya Rais kupitia Mfuko wa TASAF hivyo matumizi sahihi ya fedha yajidhihirishwe katika mradi huu,” Amesema Jenista.
Waziri huyo pia ametoa wito kwa wataalam kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa hasa maafisa wa Idara ya Ujenzi, Manunuzi na Fedha ili kuepuka kusuasua kwa mradi huo pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji katika ngazi zote kuanzia hatua ya awali hadi hatua ya mwisho ya ukamilishaji wa mradi.
“TASAF ni chombo cha Serikali ambacho kinasaidiana na vyombo vingine kusaidia jitihada za kuondoa kero ya umaskini, upatikanaji wa maji safi na salama, elimu na afya ili kujenga Jamii iliyo bora, ambayo sisi sote ni mashahidi. TASAF imeleta mafanikio makubwa katika Nchi yetu kama ilivyoainishwa katika Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa 2020/2025 kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji wa Jamii,”amebainisha Waziri huyo.
Akitoa taarifa ya Shughuli za TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe amesema kukamilika kwa ujenzi wa Stendi hiyo ya mabasi utarahisisha usafiri kwa wananchi watakaofika katika Halmashauri hiyo kupata huduma.
“Faida nyingine ni Mazingira bora kwa wafanyabiashara eneo la stendi, kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo la stendi kwa wasafiri na wafanyabiashara , kuongezeka kwa pato la Halmashauri , kuongeza fursa ya ajira kwa vijana na wananchi pamoja na huduma ya usafiri kwa wanaosafiri kutoka nje na ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea,” ameeleza Mkurugenzi huyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Shedrack Mziray ameeleza kuwa Mfuko huo umekuwa ukitekeleza miradi ya maendeleo nchini kwa lengo la kukwamua Kaya masikini na hatimaye waweze kubuni na kuanzisha miradi yao binafsi ili kumudu gharama za maisha.
“Tunafanya utekelezaji katika maeneo manne Kitaifa tunafanya Uhawilishaji wa fedha ambapo mpaka sasa tumehawilisha shilingi Bilioni 919.6 tangu kuanza kwa Awamu ya kipindi cha Pili mwaka 2020 na kufikia kaya zaidi ya Milioni 1.3. Pia tumefanya miradi ya ajira za muda karibu miradi 14,236 yenye thamani ya Bilioni 169 na kutoa ajira kwa Kaya zaidi ya 660,000 pamoja na miradi ya kukuza uchumi wa kaya,” Amesema
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini Menas Komba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa huku akiipongeza TASAF kwa kuanzisha mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi katika Kijiji cha Lundusi ambapo kukamilika kwake kutainua vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Social Plugin