WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza washindi wa Tuzo ya watafiti wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa hafla iliyofanyika leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma.
SEHEMU ya Washiriki wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, wakati akitangaza washindi wa Tuzo ya watafiti wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa hafla iliyofanyika leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma.
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe,akizungumza wakati wa kutangazwa kwa washindi wa Tuzo ya watafiti wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa hafla iliyofanyika leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma.
MWENYEKITI wa Kamati ya tuzo ya watafiti wanaochapisha tafiti zao katika Majarida yenye hadhi ya Juu Kimataifa,akitoa Tathmini ya Machapisho kwa ajili ya utoaji Tuzo kwa Watafiti wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu Kimataifa hafla iliyofanyika leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwatangaza washindi wa Tuzo ya watafiti wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa hafla iliyofanyika leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WASHINDI watafiti 47 kutoka taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi wametunukiwa tuzo kwa kuchapisha tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa ili kuchochea utafiti wa kisayansi nchini.
Akizungumza leo Septemba 16,2023 jijini Dodoma Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,amesema chapisho lililofikia vigezo linapata Sh.Milioni 50 ikiwa ni motisha kwa watafiti kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia.
“Hawa watagawana fedha iliyotengwa Sh.Milioni 500 kwa vigezo husika, tunataka wahadhiri wetu wafanye utafiti utakaosaidia kwa maendeleo ya taifa,”amesema Prof.Mkenda
Ameongeza kuwa “Sisi tuna haja ya kuwawezesha wanasayansi wetu katika utafiti kutatua matatizo yetu, tunachokifanya ni kidogo lakini kinatuma salamu, tunataka mtafiti aweze kuchuma maisha yake kutokana na utafiti.”
Waziri Mkenda amesema fedha walizopata zitachagiza kujikita kwenye utafiti wenye tija kwa taifa na kujikwamua kiuchumi.
“Tunataka wajikite kwenye utafiti na si kukimbilia kufuga kuku, kufungua baa ili kupata fedha tunataka waende kwenye majarida hayo ili utafiti wao ujiuze na utawezesha wao kujikwamua kiuchumi,”amesema Prof.Mkenda
Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda alizindua dirisha dogo la kuwasilisha machapisho hayo yaliyochapishwa ndani ya kipindi cha mwezi Julai mosi 2022 hadi Mei 31, 2023 ambapo mwisho wa kuwasilisha ni Oktoba 31, 2023.
Amesema katika tuzo hizo yameongezwa maeneo mengine ambayo ni sayansi ya mifugo na kilimo, uhandisi na Tehama.
Aidha Waziri Mkenda amesema wizara hiyo inapima matokeo ya watafiti wa ndani kulingana na kazi zao zinazo chapishwa katika majarida makubwa ulimwenguni.
"Ili uwe Mkubwa lazima upimwe ama ushindanishwe na Watu wa kubwa ndio maana tumewapima watafiti wetu Kwa kuangalia machapisho yao yaliyochapishwa katika majarida makubwa ulimwenguni,"amesema Mkenda
Baadhi ya washindi katika Tuzo hizo ni Prof.Herzon Nonga kutoka Taasisi ya Sokoine University of Agriculture,Prof.Abel Makubi kutoka Taasisi ya Muhimbili University Of Health and Allied,Prof.Reginald Kavishe kutoka Taasisi ya Kilimanjaro Christian Medical University College,Dk.Franco Peniel Mbise Taasisi ya University Of Dodoma.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Tathmini ya Machapisho kwa ajili ya utoaji tuzo kwa watafiti wanaochapisha matokeo ya utafiti wao kwenye majarida yenye hadhi ya juu kimataifa, Prof.Yunus Mgaya, amesema machapisho 82 yaliokelewa na kamati hiyo kutoka kwa watafiti wa taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi kwenye maeneo ya afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati.
“Baada ya mchakato kukamilika machapisho 20 ambayo kati yake 10 ni mkondo wa sayansi asilia na hisabati na 10 kutoka mkondo wa afya ya sayansi tiba yamekidhi vigezo vya kupata tuzo,”amesma Prof.Mgaya
Amefafanya kuwa ndani ya machapisho hayo kuna watanzania 47 ambao wamekidhi kupata tuzo hizi zinazogharimu Sh.Milioni 500 .
Hata hivyo ameeleza kuwa serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 ilitangaza kuwa machapisho yaliyofanywa na watanzani na kuchapishwa kwenye majarida ya kimataifa ya kiwango cha juu itatoa Sh.Milioni 50 kwa kila chapisho.
A''Machi 26 mwaka huu lilifunguliwa dirisha la kuwasilisha machapisho hayo na kufungwa Mei 31, mwaka huu.''amesema