Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 20,2023 jijini Dodoma kuelekea Siku ya maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yanatarajia kufanyika Septemba 25 hadi 30 mwaka huo jijini Mbeya.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Adam Shaibu (kulia) akieleza jambo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Rasheed Maftah.
Na-Alex Sonna - Dodoma.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi za Umma kuhakikisha zinakuwa na wataalam wa lugha ya alama ili inapohitajika kutoa huduma kwa wateja wenye Uziwi pasiwe na kikwazo katika kuwasiliana.
Wito huo umetolewa leo Septemba 20, 2023 jijini Dodoma na Waziri Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuelekea Siku ya maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yanatarajia kufanyika Septemba 25 hadi 30 mwaka huo jijini Mbeya.
"Malengo ya Serikali ni kuhakikisha Kila taasisi inakuwa na wataalam wa Lugha ya alama hivyo Miongozo imeandaliwa ni vyema kila taasisi ihakikishe watu wote Wenye Ulemavu wanajumuishwa katika Fursa zote za maendeleo,"amesema Prof.Ndalichako
Aidha Prof.Ndalichako amesema maadhimisho hayo yametokana na mahitaji na changamoto zilizokuwa zinawakabili Viziwi Duniani ndio maana ikatengewa wiki yake ambapo hufanyika Kila Mwaka wiki ya mwisho ya Mwezi Septemba.
"Serikali ya Tanzania inaungana na Viziwi wote Duniani katika maadhimisho ya Wiki hii na tunahimiza matumizi ya Lugha ya alama na ndio maana kauli Mbiu ya wiki hiyo Inasema "Dunia ambayo popote walipo Viziwi wanaweza kutumia Lugha ya alama"amesema Prof.Ndalichako
Hata hivyo amewataka Wananchi kuendelea kuwathamini watu Wenye Ulemavu kwani wameshathibitisha kuwa Ulemavu wao sio kikwazo katika shughuli za maendeleo.
"Nitoe rai kwa wananchi wenzangu wa Tanzania kuwathamini na kuziunga mkono kazi zinazofanywa na Watu Wenye Ulemavu kwani wameshathibitisha kuwa sio kikwazo katika shughuli za maendeleo,"
Aidha amefafanua lengo la kuanzishwa kwa wiki ya Viziwi Duniani ni kutoa fursa Watu wa Jamii ya Viziwi kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za Maendeleo kwa kushirikiana na jamii zinazowazunguka bila kuwepo vikwazo vyovyote ikiwemo vikwazo vya mawasiliano yao.
''Serikali inayoongowa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa Watu wenye Ulemavu nchini ikiwa ni pamoja na Watu wa Jamii ya Viziwi ambapo elimu imeendelea kutolewa kwa umma na wadau mbalimbali kuhusu changamoto zinazo kabili kundi hilo ikiwemo kuhamasisha utamaduni wa kuwasiliana kwa kutumia lugha ya alama.''amesema
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Adam Shaibu ameishukuru serikali kwa kutoa ushirikiano na kuwamini Watu wenye Ulemavu ikiwemo kuwapatia fursa za kiuchumi, kijamii, kiuongozi na ajira.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu 2023 ni “Dunia ambayo Popote Walipo Viziwi Wanaweza Kutumia Lugha ya Alama.”
Kauli mbiu hii inalenga kila taasisi inayotoa huduma kwa jamii inakuwa na mkalimani wa lugha ya alama sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wake kuwa na uelewa wa lugha ya Alama.