Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SILAA ATAKA SIKU MIA MOJA KUTUMIKA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Dkt Angeline Mabula katika ofisi za wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma tarehe 4 Sept 2023.

******************

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ameelekeza watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha ndani ya siku mia moja kuanzia sept 4, 2023 wanatatua migogoro ya ardhi kwa kadri ya uwezo wa nafasi zao.

Aidha, ametaka waliovamia maeneo ya wazi kuanza kuondoka mara moja huku akielekeza viongozi na watendaji wa wizara ya ardhi wenye mamlaka ya kusimamia sheria kuhakikisha ndani ya siku hizo mia moja maeneo hayo yanakuwa wazi.

Waziri Silaa ametoa kauli hiyo wakati akizumgumza na Menejiment ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mara baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Dkt Angeline Mabula tarehe 4 Sept 2023 katika ofisi za wizara hiyo eneo la Mtumba Dodoma.

"Nawaomba na kuwaelekeza watendaji wote ambao sheria imewapa mamlaka kwa kiasi chao cha kutatua migogoro ndani ya siku hizi mia moja atatue kwa kadri ya uwezo wake.

Waziri huyo wa Ardhi amewataka pia watendaji wa sekta ya ardhi kusimamia haki halali wakati wa kutekeleza majukumu yao bila kujali sura wala rangi huku akionya wanaotumia fedha kunyima haki za wengine.

Silaa alielezea pia suala la migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa, maelezo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utatuzi wa migogoro ya àrdhi katika maeneo wanayoishi wananchi ni lazima busara itumike.

"Mhe Rais ameelekeza katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ambayo wananchi wanaishi busara itumike, kwa sababu wale ni watu na wakati mwingine maamuzi yakifanyika kuwaondosha athari inaweza kuwa kubwa kuliko faida, naomba hilo mlizingatie" alisema Silaa.

Akigeukia suala la ufanisi kazini, Silaa ametaka mabadiliko makubwa katika utendaji ili kuleta ufanisi wa kazi huku akiahidi kuwepo mifumo mizuri itakayohakikisha kazi wanazofanya watendaji zinapimika, kuelekezeka sambamba na kuifanya serikali ya CCM imeweza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Kuhusu mifumo ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema amesikitika kuona watu wakielezea matumizi ya mifumo huku wananchi wakiendelea kwenda kwenye ofisi kuhitaji baadhi ya huduma za mifumo hiyo.

"Tunafanya kazi in a primitive way, kazi very manual na tukiendelea hivyo efficiency ya wizara itazidi kupungua na huku tunakoelekea tutaipeleka nchi katika eneo baya, tuna kazi ya kufanya, tuwe na modern ICT system tu na tuwe modern app ili watu waweze kuzungumza na wizara na kujiona huru’’ alisema Silaa.

Pia alielezea suala la vituo vya mafuta na kubainisha kuwa ipo Kanuni ya Mwaka 2018 inayotaka kituo cha mafuta kiwe umbali wa mita za mraba 400 yaani mita 20 kwa 20 na kuweka kuwa kuanzia tarehe 1 sept 2023 wote walioomba kinyume na kanuni hiyo maombi yao yasimamishwe watakapokutana na kushauriana.

Awali wakati wa makabidhiano ya ofisi aliyekuwa Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alisema, alipoingia na anapoicha wizara hiyo ana imani iko kwenye hali nzuri zaidi na ni imani yake Waziri Silaa atakuwa hana changamoto nyingi kama alivyozikuta wakati anakabidhiwa wizara.

‘’Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan sekta ameisogeza vizuri na tunakwenda na tukumbuke ameifungua nchi uwekezaji unakuja kwa kasi na sisi kama wizara ndiyo tunamiliki ardhi’’ alisema Dkt Mabula.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula akizungumza mara baada ya kukabidhi ofisi kwa waziri wa wizara hiyo Jerry Silaa tarehe 4 Sept 2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto), Naibu Waziri Geofrey Pinda (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kulia) na Naibu Waziri Lucy Kabyemera mara baada ya makabidhiano ya ofisi jijini Dodoma tarehe 4 Sept 2023.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula (kulia) akiagana na aliyekuwa Naibu wake Geofrey Pinda. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com