Na Mwandishi Wetu
Uongozi wa Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) ambao ndio wadhamini wakuu wa Klabu ya Geita Gold FC. yenye maskani yake mkoani Geita wamekabidhi basi lenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kwa Klabu ya Geita Gold leo Mkoani Geita.
Akikabidhi basi hilo kutoka kwa Uongozi wa GGML leo mjini Geita, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameutaka Uongozi wa klabu hiyo pamoja na wachezaji kuongeza bidii katika kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo zinawapa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri.
"Niwapongeze tena ndugu zangu wa GGML kwa kukubali kuifadhili timu yetu ya GGFC, lingekuwa jambo la ajabu sana katika mkoa huu unaofahamika kwa uzalishaji wa dhahabu alafu mkakosa timu ambayo haina ufadhili imara kama yalivyo maeneo mengine, " amesema Waziri Mavunde.
Mavunde amesema ni klabu chache ambazo zinamiliki mabasi ya kusafiria na huku akiupongeza mgodi wa GGML kuendelea kuchangia maendeleo kwa wana-Geita huku akisisitiza kukamilisha uwanja unaojengwa kata ya Magogo kwa ajili ya shughuli za kimichezo.
Akizungumzia mchango wa GGML kwa timu hiyo Mkurugenzi Mtendaji GGML, Terry Strong amesema ushirikiano uliopo kati yao na Klabu hiyo ya soka unatoa picha halisi kwamba ni zaidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwani unajumuisha umoja, uthabiti na moyo wa unyenyekevu kwa jamii ya Geita.
Amesema GGFC imewatia moyo kwa jitihada inazoonesha katika michuano mbalimbali kuanzia makocha wake, wachezaji na watu waliojitolea kuishika mkono timu hiyo ni dhahiri wameonyesha nguvu ya pamoja, kazi ya pamoja na shauku ya mafanikio ya timu hiyo ndani na nje ya uwanja.
“Nina furaha kutangaza mchango muhimu GGML kwenda GGFC. GGML imetoa msaada wa basi hili jipya kabisa lenye viti 45 kwa timu hii.
“Basi hili linawakilisha zaidi ya chombo cha usafiri, kwani linakuwa mfano wa kujitolea kwetu kwa maendeleo ya klabu yetu ya soka ndani na nje ya jamii ya Geita pia basi hili litasaidia wachezaji na wafanyakazi kuhudhuria michezo na mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya fursa ambazo labda hawakupata,” amesema.
Aidha, ameishukuru jamii ya Wana-Geita na Tanzania kwa ujumla kwa imani yao kwa GGML na kuwa msingi wa mafanikio hayo.
“Tumejitolea kudumisha ushirikiano wetu kwenu nyote. Tumejitolea kukuza uhusiano huo na kufanya kazi pamoja ili kuendeleza jamii yenye ustawi na umoja,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Mji Geita kupitia Mkurugenzi wake kuhakikisha wanakamilisha mapungufu yote yaliyojitokeza kwenye jezi za mpira zilizotolewa na Uongozi wa GGML.
Ikumbukwe kuwa Mgodi wa Geita Gold Mining ambao ndio wadhamini wakuu wa klabu hiyo wamewekeza kiasi cha Shilingi Milioni 800 kama wadhamini wakuu wa klabu Hiyo.
Social Plugin