SHERIA YA LOCAL CONTENT INAVYONUFAISHA WAWEKEZAJI WAZAWA GGML


Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kushoto) na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo (kulia) wakipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Blue Coast.
Mabasi ya kampuni ya Blue Coast yanayotumika kusafirisha wafanyakazi na wakandarasi wa GGML.
Mmiliki wa kampuni AKO Group, Silvestry Koka akizungumza katika kongamano la wachimbaji madini mkoani Geita.
Mmoja wa wafanyakazi wa AKO Group akimhudumia mmoja wa wateja waliofika katika banda la kampuni hiyo kwenye maonesho ya teknolojia ya madini Geita.


NA MWANDISHI WETU
Miaka mitano baada ya kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Uwezeshaji Wazawa (Local Content) mafanikio yameanza kuonekana kuwa lulu kwa Watanzania huku fursa za ajira zikizidi kufunguliwa.

Sheria hiyo ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inalenga kutoa fursa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.

Mafanikio hayo yameelezwa katika Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini Geita wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini kujadili fursa za uwekezaji kupitia sheria hiyo lililofanyika katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 1, 2023 katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.

Kamishna wa ‘Local Content’, Janeth Lukeshingo anasema ajira zimeongezeka, manunuzi ya bidhaa na huduma kwa Watanzania, ushirikishwaji na uhaulishaji wa teknolojia na utafiti, maendeleo na kuongezeka kwa uelewa kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika seta ya madini.
Mratibu wa Local Content katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) Riwald Tenga, anasema wanatekeleza sheria hiyo kwa asilimia 90.

“Tunafuata masharti yote katika manunuzi na katika utoaji ajira, yote tunayofanya kwenye Local Content tuko kati ya asilimia 60 mpaka 90,” anasema Tenga.

AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya GGML, hivi karibu ilitoa kandarasi ya usafirishaji wa mafuta, yenye thamani ya takriban Sh bilioni 25 kwa mwaka kwa wakandarasi wawili wa Tanzania.
Miongoni mwa makampuni ya ndani yaliyonufaika ni pamoja na Blue Coast Investment Limited, kampuni ya Geita inayojishughulisha na usafiri na usafirishaji.

WAWEKEZAJI WAZAWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Blue Coast, Ndahilo Athanas anasema wameanza kufanya biashara na GGML tangu mwaka 2021.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa sheria hii na kuipitisha, lakini tunamshukuru zaidi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hii.

“GGML wana mchango mkubwa wa kutufikisha hapa tulipo, wamekuwa chachu ya sisi kufikia viwango vya ubora. Wametupatia elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa ubora na namna ya kuendelea kufanya biashara endelevu,” anasema Athanas.

Anasema wanaendesha shughuli zao kupitia viwango vya kitaifa na kimataifa ambapo wana cheti cha usalama kazini, cheti cha ubora wa kazi na sasa wanaendelea na usajili wa ubora katika usimamizi wa mazingira.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 400 kwenye ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wakazi wa Geita na maeneo mengine yanayozunguka mkoa huo na kufanya idadi kufikia 580 kutoka 220 wa mwaka 2021.

Aidha, anasema wamejikita kutoa elimu kazini ili kuwajengea uwezo vijana kabla ya kuwapa ajira rasmi hasa wahitimu wa vyuo vikuu.

“Mpaka sasa vijana 50 wameajiriwa kupitia utaratibu huu katika nyanja mbalimbali kama uhasibu, maofisa ugavi, mafundi magari, maofisa uendeshaji na nyingine,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema pia wamepata tuzo ya mlipakodi bora kwa Mkoa wa Geita na kwamba kupitia fursa ya Local Content kampuni hiyo imekua na sasa imehamishiwa kwenye kundi la walipakodi wakubwa.

AKO

Ako ni kampuni iliyoanzishwa kutoa huduma ya chakula. Ni moja ya kampuni ya wazawa ambayo ilianza mahusiano GGML mwaka 2010.

Mmiliki wa kampuni hiyo, Silvestry Koka anasema walianza kwa kutoa huduma za chakula kwa GGML ambapo wakati huo walikuwa wanachukua bidhaa za kupika na mahitaji mengine kutoka Dar es salaam.

“Lakini wakati huo tulikuwa tunaendelea kuwajengea uwezo wananchi wanaozunguka maeneo yote yanayokaliwa na mgodi,” anasema.

Anasema sasa AKO inajivunia kwa kuwapa mnyororo wa uchumi wananchi wanaozunguka eneo la mgodi.
Kwamba wamewasaidia kuwa soko kubwa la bidhaa zao za mbogamboga, matunda na bidhaa zingine pia.

“Kwahiyo tumekuwa tukinunua kwa asilimia kubwa, japo kuna bidhaa tunazitoa nje ya hapa Geita. Lakini lengo letu tufikie hatua bidhaa zote kwa asilimia 100 zitoke katika maeneo yanayozunguka mgodi.

“Tunatumia nyama, mchele, matunda na mbogamboga, kwa mfano kuna kikundi kinaitwa NYAKABALE Commercial group ambacho wao wanatusambazia nyama, matunda pamoja na mbogamboga lakini pia tunaye mzabuni wetu anaitwa Masuka, MASUKA ambaye amekuwa ana supply mchele kwetu kwa zaidi ya miaka nane mpaka sasa,” anasema.

Aidha, Koka anatoa wito kwa watoa huduma wazawa kufanya kazi kwa kusimamia kampuni zao na kuzipa Zaidi uwezo poamoja na kuzingatiwa viwango.

Anasema kinachoangusha kampuni nyingi za wazawa ni kuangushana wao wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo si afya kwa uchumi wa Taifa.

DHANA YA LOCAL CONTENT

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, anasema dhana ya Local Content ilikuwa mpya wakati tume hiyo inaanzishwa lakini hivi sasa imeanza kueleweka.

“Watu waliturushia matusi kuhusu Local Content lakini kwa sababu kuna watu walikuwa hawajaielewa lakini tumefikia mahali ambapo panastahili,” anasema Profesa Kikula.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, amesema baada ya marekebisho ya sheria hiyo wameanza kuona manufaa na kuipongeza Serikali kwa kuisimamia.

“Baada ya kuanza kutekelezwa kwa Local Content hasira ya wananchi imepungua, wengi wanashiriki, wanajishughulisha na uuzaji na usambazaji wa bidhaa wenye migodi mbalimbali,” anasema Kanyasu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela anashauri uzoefu uliopatikana katika sekta ya madini uendelezwe katika sekta nyingine.

“Tukifanya hivi itatusaidia kuendeleza ujuzi na uelewa kwa Watanzania ili wengi zaidi washiriki katika sekta nyingine,” anasema Shigela.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo anasema ndani ya muda mfupi ushiriki wa Watanzania umeongezeka katika sekta ya madini.

“Tumejifunza kuna mambo lazima twende tukayafanyie kazi kwa haraka, Local Content inagusa maisha na uchumi wa Watanzania.

“Profesa Kikula moja ya alama ambayo utaiacha tena katika mioyo ya Watanzania na hasa wadau wa sekta ya madini ni namna ulivyosimamia Sheria ya Local Content…matokeo tumeanza kuyaona,” anasema Mavunde.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post