Adela Madyane-Kigoma.
Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Itebula kinachojishughulisha na zao la tumbaku wilayani Uvinza mkoani Kigoma Kayaya Josephat, alisema wanawake wengi wanashindwa kushiriki katika kilimo cha tumbaku kwasababu wengi wao hawamiliki mali zisizo hamishika kama nyumba na ardhi huku wengine wakishindwa kulima kwasababu ya kukosa mwamko juu ya faida ya zao hilo.
Josephat alisema katika chama chake cha msingi chenye wakulima 60, wakulima wanawake ni wawili tu na walio salia wote ni wanaume na kuwataka wanawake kushiriki katika zao hilo la biashara kwaajili ya kujiongezea kipato kitakachowanufisha wao na familia zao.
“Wanawake wengi huona kazi ya tumbaku kuwa ni ngumu na ni ya wanaume, lakini wengine wanashindwa kujiunga kwakuwa wanakosa dhamana ya mali isiyohamishika, wanawake wengi hawamiiki mali, wengi wao wanashiriki kupitia waume zao hivyo kushindwa kupata faida za moja kwa moja, mimi niwatoe hofu wajiunge kwenye vikundi vya ushirika waanze kulima kwakuwa zipo samani nyingine za kuweka dhamana si lazima nyumba na shamba”, amesema Josephat.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha msingi Matabalo Boaz Ntanda, kilichopo kata ya Nyakitonto halmshauri ya wilaya ya Kasulu alisema kati ya wanachama 160 wa chama chake wanachama wanawake ni wanne tu huku akitaja sababu kuwa wanawake wengi wanasema tumbaku inahitaji mtaji mkubwa tofauti na mazao ya mahindi na maharage mtaji ambao wanawake wengi hawana.
Akiwatoa hofu wanawake wenzie Tiba Haruna ambaye ni mkulima wa chama msingi cha Mugwezi alisema, zao la tumbaku limemuwezesha kukuza uchumi wake, ambapo alianza kulima hekali moja mwaka 2017 na sasa analima hekali nne na kuwataka wanawawake kutoa dhana potofu kwamba kilimo hicho kinawafaa wanaume pekee kwani pesa haichagui mwanamke wala mwanaume cha muhimu ni kupambana.
“Mimi kama mama namshukuru Mungu zao la tumbaku limeniinua sana, nililima mazao mengine kwa muda mrefu ila sikufanikiwa kama nilivyofanikiwa kupitia zao hili, nimesomesha mtoto mpaka chuo kikuu, nimejenga nyumba na nina kula vizuri kupitia zao hilo, naomba wananwake wenzangu wasiogope, wajikite katika kilimo cha zao la tumbaku kwani kina pesa na faida kubwa cha msingi ni kufuata taratibu za kilimo kama zinavyoelekezwa na maafisa ugani”
Naye Scholastika Fabian mkulima wa chama cha msingi Matabalo alisema, yeye alianza kulima zao hilo baada ya mume wake kufariki na kumuacha na watoto tisa na kwamba toka amejikita katika kilimo hicho hajawahi kupata changamoto ya malezi ya watoto kwakuwa kupitia kilimo hicho amezeweza kujenga nyumba yake Kasulu mjini yenye thamani ya takribani milioni thelathini na anawatunza watoto vizuri akiwapatia huduma zote za msingi.
Zabina Mussa katibu wa chama cha msingi Matabalo alikubaliana na hali halisi kuwa, zao la tumbaku linahitaji kuwa na nguvu ya kifedha na hivyo kutoa rai kwa wanawake kuwa ili kukabiliana na changamoto ya kipato inawapasa kujiunga katika vikundi mbalimbali hususan vya kilimo ili kujua fursa zilizopo na waweze kukopesheka kwani hata yeye alikopa milioni tano na kuanza kilimo hicho na baada ya mavuno alipata zaidi ya milioni 20 zilizomuwezesha kulipa deni na kujenga nyumba kwa milioni 15.
“Fursa haziwezi kukuta ukiwa umekaa nyumabani na huwezi kupata mkopo ukiwa mmoja mmoja, pesa zinatolewa kwa vikundi, ukiwa nyumbani kama mwanamke huwezi kupata ila ukiingia kwenye kikundi unapata pesa, unafanya kazi kwa uhuru na mwisho wa siku unapata pesa za kuendeleza maisha ya kila siku” ,amesema Mussa.
Caption 01. Mwanamke Tiba Haruna wa chama cha msingi Mgwezi lilichopo wilayani Uvinza aliyejishughulisha na kilimo cha tumbaku na kupata faida ya kusomesha watoto na kujenga nyumba.
02. Mwanamke Zabina Mussa wa kata ya Nyakitonto wilayani Kasulu aliyeshiriki kilimo cha tumbaku kwa msimu wa 2022/2023 na kupata faida iliyomuwezesha kujenga na kulipa deni alilokopa kwenye kikundi kwaajili ya kuendesha shughuli za kilimo.