Mhandisi Mkuu Sinohydro Co. Ltd, Bw. Daniel Xhu akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (kulia)
Eng. Emmanuel Anderson Meneja Mradi wa Umeme Jua (MW 50) - Kishapu Tanesco akielezea kuhusu mradu wa Umeme Jua
Na Mwandishi wetu - Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme ameitaka Kampuni ya Sinohydro Company Limited iliyopewa kandarasi ya kujenga Mradi wa Umeme wa Jua wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 323 unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kukamilisha ujenzi huo kwa wakati, kwa kuzingatia ubora, viwango, muda waliokubaliana na bila kuongeza bajeti ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya uhakika ya umeme.
Mhe. Mndeme amemuagiza Mkandarasi huyo leo tarehe 29 Oktoba, 2023 alipokuwa akizungumza na wadau wa mradi , baadhi ya wananchi waliopisha mradi katika kijiji cha Ngunga, viongozi mbalimbali, pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Tanesco huku akimsisitiza kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wa Ngunga, Kishapu na Shinyanga kwa ujumla katika mradi huu muhimu.
"Nikuombe (Sinohydro Co. Ltd) mkandarasi uliyepewa dhamana ya kujenga mradi huu mkubwa wa umeme hapa kijiji cha ngunga Kishapu, ukamilishe mradi huu kwa wakati na kwa kuzingatia muda, viwango, thamani na bajeti tuliyokubaliana ili wananchi waanze kunufaika na uwepo wa mradi huu," amesema Mhe. Mndeme.
Awali akiwakaribisha wadau wa mradi huo ambao ni Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD group - Dar es salaam Agency aliwaeleza kuwa serikali itafanya kazi nao bega kwa bega, itawapatia ushirikiano wakati wote na pia aliwashukura kwa ujio wao kuja kuona eneo litakalotekelezwa mradi huo mkubwa wa umeme.
Mhe. Mndeme kipekee kabisa amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mradi huo mkubwa wa umeme ha hasa kuja kutekelezwa katika kijiji cha Ngunga kilichopo Wilaya ya Kishapu hapa mkoani Shinyanga, mradi wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 323 fedha za kitanzania.
"Kutekelezwa kwa mradi huu kunakuja kuondoa kabisa changamoto za nishati ya umeme, kuongeza ajira hasa kwa wanashinyanga na kuimarisha uchumi wa wananchi wetu, na haya ndiyo malengo ya Mhe. Rais wetu kwa watanzania kuwaondolea kero zote na kuimarisha uchumi wao," amesema Mhe. Mndeme.
Akitoa salamu za AFD Group Bw. Philippe Micheud ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo Ufaransa AFD Group Dar es salaam Agency amesema kwamba, yeye na timu yake wameridhishwa na maandalizi yaliyowekwa katika kutekeleza mradi huo na kwamba wamevutiwa na kuridhishwa na eneo lililotengwa katika utekelezaji wa mradi kwa ujumla wake.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Umeme Jua ( MW 50 ) Ngunga Kishapu Mhandisi Emmanuel Anderson amesema, wao kama Tanesco wamejipanga vyema sana katika kusimamia na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, kwa viwango na kwa kuzingatia thamani ya fedha ili kuweza kufika lengo la serikali na watanzania kwa ujumla kwa kupata nishati ya umeme iliyokusudiwa na kwa wakati.
Naye Bw. Tonny Du ambaye ni Meneja Mradi wa Sinohydro Cp. Ltd alimueleza Mhe. Mndeme na ujumbe wote alioambatana nao kuwa, wao wamejipanga vyema kuutekeleza mradi huu na kukabidhi kwa wakati kwa kuwa uwezo huo wanao na vifaa wanavyo.
Huu ni mradi wenye jumla ya megawati za umeme 150 ( MW 150 ) unaotekelezwa kwa awamu, ambapo kwa sasa wanaanza na megawati 50 na kisha kufuatiwa na megawati 100 nyingine na unakadiriwa kugharimu takribani Bilioni 323 fedha za kitanzania.
Mradi unachukua eneo la zaidi ya hekari 1000, ambapo wananchi 110 wamepissha utekelezwaji wa mradi huu, na kwamba mkandarasi wa Kampuni ya Sinohydro amesaini mkataba wa miezi 17 ambapo ndani yake ipo miezi 3 ya kuanza kufanya kazi baada ya kukamilika kwa mradi kabla ya kukabidhi mradi huu rasmi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza
Philippe Micheud Naibu Mkurugenzi AFD Group Dar es salaam Agency Tanzania akizungumza
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameitaka Kampuni ya Sinohydro Co. Ltd. iliyopewa kandarasi ya kujenga Mradi wa Umeme wa Jua wenye thamani ya zaidi ya Bil. 323 ktk kijiji cha Ngunga - Kishapu kukamilisha ujenzi kwa wakati,ubora, viwango kwa muda waliokubaliana pic.twitter.com/7IPIvUpZIs
— Malunde 1 Blog (@malundekadama) October 29, 2023
Social Plugin