Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMEND WAKAMILISHA MRADI WA USALAMA BARABARANI TANGA, UONGOZI WA JIJI WATOA SHUKRANI

Naibu Meya wa Jiji la Tanga  Rehema Kasimu( wa pili kushoto) akimpatia cheti cha kutambua mchango wa Mwalimu wa Shule ya Msingi Usagara Faraja Mwajike kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya usalama barabarani. Kushoto ni Meneja wa Amend Tanzania Simon Kalolo akishuhudia tukio hilo.

**************

Na Mwandishi Wetu, Tanga

UONGOZI wa Halmashauri ya Jiji la Tanga umetoa shukrani kwa Shirika la Amend baada ya kukamilisha Mradi wa Usalama Barabarani kupitia Mradi wa Tanga Yetu uliowezesha wananchi wa Jiji hilo kupata elimu ya usalama barabarani.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mradi huo ambao ulianza mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2023, Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shillow amefafanua kipindi cha miaka minne wamekuwa na Amend katika kushirikiana kuhusiana na suala zima la usalama barabarani.

“Amend ni miongoni mwa mashirika yanayofanya kazi kwa ukaribu katika program ya Tanga Yetu , ni miongoni mwa miradi 17 tuliyokuwa nayo katika miradi ya Tanga Yetu na moja ya mradi huo ni mradi wa usalama barabarani.Katika mradi huu waliokuwa wamepata kazi ya kuusimamia na kuendesha ni Amend.

“Mradi huu umefika mwisho na umefanyika kwa miaka minne ukiwa unafadhiliwa na Shirika la Botnar chini ya mradi wa Tanga Yetu na leo tumekuja kuwapa taarifa wadau tuliokuwa tunashirikiana nao tangu mwanzo."

Amefafanua mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka hiyo minne kwa kuhakikisha elimu ya usalama barabarani imetengamaa na imejitosheleza katika jiji la Tanga, kwasababu mradi huu pia uligusa uboreshaji wa miundombinu.

Pia wameboresha miundombinu katika Shule ya Msingi Usagara, Chuda, Mwazange na Mabawa katika maeneo mahususi ambayo watoto wanaweza kupita kwa usalama na kuepuka kupata ajali za barabarani.

“Elimu hiyo imetolewa ya kutosha katika Jiji la Tanga na zimetolewa kwa nyakati tofauti lakini hawakuishia hapo wametoa elimu kwa madereva zaidi ya 900 ambao nao walipewa elimu sahihi ya matumizi ya barabara lakini jinsi gani ya kumlinda mtumia barabara ili na yeye awe salama.”

Ameongeza kikubwa ambacho Amend walikifanya ni kuanzisha Mahakama Kifani ya Watoto iliyokuwa ikiendesha kesi za madereva waliovunja sheria za usalama barabarani na madereva hao walihukumiwa.

Meya Shillow amesema Mahakama ya Watoto imewasaidia watoto hao kuwa na ujasiri na kufahamu haki zao kuwa sheria za barabarani zipo na zinatakiwa zifuatwe na zinaweza kutolewa hukumu na watu wakahukumiwa.

Pia amesema kupitia mradi huo kumekuwepo na mafunzo ya kuwajengea uelewa wananchi. “Jambo la kufurahisha mradi huu umekwisha lakini Amend wamepata mfadhili mpya wa Serikali ya Uswiss ambao wameona umuhimu wa kuendelea na Amend katika Jiji la Tanga na Dodoma.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema mradi umefanikiwa kubadilisha mtazamo wa viongozi wa juu wa Jiji la Tanga kuhusu usalama barabarani.

“Kwa muktadha wa mradi huu, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wadau na wakala mbalimbali kukutanishwa kuchangia maoni yao kuhusu usalama barabarani. Utengenezaji wa Mpango Kazi wa Usalama Barabarani kwa Jiji la Tanga uliofanywa na Amend …

“Mpango huo ni wa kwanza kabisa wa aina yake kwa Tanga.Umeweka dira ya usalama barabarani ya 2023-2030 na kuainisha mikakati ya kufanikisha hili.

“Pia unatumika kama ramani ya barabara kwa wadau wa usalama barabarani Tanga katika maendeleo ya sera (halmashauri ya jiji) na utekelezaji (wahandisi na trafiki).”

Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo amesema tangu ulipoanza mwaka wa 2019 mpaka mwaka 2023 pamoja na mambo mengine kumefanyika uboreshaji wa miundombinu katika shule za msingi 11, ikiwa ni pamoja na njia za miguu, madaraja ya waenda kwa miguu, alama za barabarani, matuta, alama za pundamilia, na zaidi;

Amesema Amend kwa kushirikiana na Kikosi cha usalama barabarani wameendesha mafunzo kwa waendesha pikipiki zaidi ya 900 huku pia wakitekeleza Mahakama ya Watoto katika shule tano za msingi (Usagara, Mwanzange & Martin Shamba, Mwenge, Mwakizaro),

Aidha wametoa elimu ya usalama barabarani kwa zaidi ya watoto 12,000 wa shule za msingi, uwezeshaji wa mafunzo kwa Polisi wa Trafiki, kampeni ya uhamasishaji wa usalama barabarani ikijumuisha kampeni ya vyombo vya habari, ujumbe kupitia kwa maofisa wa maendeleo ya jamii na ujumbe kupitia wanasiasa wakiwemo madiwani,

Pia wametoa mafunzo kwa maofisa wa Serikali 139, taasisi za elimu 14, wanafunzi 12,894, walimu 128, askari polisi 29 na madereva 1,220 wameguswa moja kwa moja na kutengeneza Mpango Kazi wa Usafiri Salama na Endelevu wa Jiji la Tanga.
Naibu Meya  wa Jiji la Tanga  Rehema Kassim (wa  pili kushoto) akimpatia cheti cha kutambua mchango wake katika mapambano ya usalama barabarani mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Old Tanga Shadia Ally.Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Amend Tanzania Simon Kalolo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com