Wakati wa ziara ya Ujumbe wa Tanzania nchini Thailand, mbali na kutembelea shughuli za madini, ulipata wasaa wa kukutana na kijana wa Kitanzania Suleiman Kilonda aliyewekeza jijini Bangkok nchini humo kwa kumiliki kiwanda cha kushona na kuchapisha fulana cha Sk Export.
Mbali na kumiliki kiwanda, Suleimani amefungua maduka ya kuuza nguo za aina mbalimbali zenye chapa zake za African Man, African Queen, Town Totoz na King Kaka ambapo ameajiri wafanyakazi wapatao 200.
Katika mahojiano maalum, Suleiman alisema malengo yake ni kufungua kiwanda kikubwa nchini Tanzania chenye uwezo wa kuajiri watanzania wengi na kutumika kama sehemu ya kujifunzia kwa kila mtanzania mwenye ndoto za kumiliki kiwanda cha nguo.
‘’ Tayari nimeshanunua sehemu ya kufungua kiwanda nchini Tanzania katika eneo la Mlandizi ramani ninayo ya aina ya kiwanda ninachotaka kukifungua lakini changamoto bado natafuta fedha za kuanza ujenzi, nimejaribu kwenda kwenye baadhi ya taasisi za fedha lakini bado sijafanikiwa. Ombi langu langu kwa Serikali ni kuniwezesha kufikia ndoto hiyo ambayo itawasaidia na watanzania wenzangu kupitia mimi,’’ alisema Seleman.
Ameongeza kuwa, malengo ni kujenga kiwanda chenye uwezo wa kuajiri watu 2,500 na uwezo wa kuzalisha nguo 100,000 kwa siku.
Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Michael Majebele alisema Mipango yake ya uwekezaji ni mzuri tija kwa taifa, kuanzia kwenye suala la ajira, kodi na kubadilishana ujuzi hivyo na kueleza kuwa, mwekezaji huyo anakaribishwa TIC ili aweze kusajili mradi wake jambo ambalo litamwezesha kufurahia vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa nchini ambavyo vitamsaidia kwenye kupunguza gharama za uanzishaji wa kiwanda chake.
Majebele aliongeza kuwa, mwekezaji huyo anashauriwa kukutana na benki yoyote ya Tanzania ili iweze kumsaidia kwenye masuala yake ya kifedha pale anapokidhi vigezo vyao walivyojiwekea.
Naye, Meneja wa Biashara kutoka Tume ya Madini, George Kaseza alimweleza kuhusu uwepo wa fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini ambazo anaweza kuzitumia ili kutanua wigo wake wa kiuwekezaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Daniel Kidesheni alitoa zawadi kutoka katika kituo hicho kama shukrani kwake ya ukarimu kwa wageni wanaomtembelea.
Kuona bidhaa zake tembelea Instagram
sk_ export na Facebook
sk_ export