Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BASHUNGWA AAGIZA UJENZI WA NJIA NNE BUKOBA KAZI UFANYIKE USIKU NA MCHANA



Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa Kagera kumsimamia Mkandarasi M/s Abemulo Contractors Ltd afanye kazi usiku na mchana ya ujenzi wa upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye) - Bukoba Port (km 5.1), sehemu ya kwanza yenye urefu wa kilometa 1. 


Bashungwa ametoa agizo hilo leo tarehe 28 Oktoba 2023 Bukoba mkoani Kagera wakati akikagua kuanza kwa kazi ya Ujenzi wa upanuzi wa Barabara hiyo ya njia nne sehemu ya kwanza inayoanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi eneo la Mitaga lenye urefu wa Kilometa 1. 

Bashungwa amesema kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango aliyoyatoa kwa TANROADS ya kukabiliana na ajali za mara kwa mara zinazotokea kwenye mteremko wa Nyangoye katika barabara hiyo. 

“Ili kutekeleza maelekezo hayo ya Makamu wa Rais, tayari Serikali Sikivu inayoongozwa na Mheshiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa Bilioni 4.61 kuanza ujenzi wa upanuzi sehemu ya kwanza inayoanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi Mitaga yenye urefu wa kilometa 1", amesema Bashungwa. 

Aidha, Bashungwa amesema atawasilisha maombi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha ujenzi na upanuzi wa njia nne katika sehemu ya kwanza ifike Roundabout ya Bukoba mjini ambapo kutakuwa na ongezeko la Mita 600 ili kuwezesha magari kufika kwa urahisi katika stendi mpya ya Bukoba inayojengwa. 

Bashungwa amesema kuwa upanuzi wa barabara hiyo katika Mji wa Bukoba unaenda sambamba na ujenzi wa miradi mingine ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa Stendi mpya ya Kisasa ya  Bukoba kupitia mradi wa kupendezesha Miji (TACTIC) na upanuzi wa Bandari ya Bukoba. 

Amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha barabara ya Rwamishenye kupitia Stendi ya Bukoba hadi Bandari ya Bukoba inapanuliwa kwa njia nne ili kurahisisha huduma ya Usafiri na Usafirishaji katika Mji wa Bukoba ambapo itasaidia kufungua mkoa huo kiuchumi. 

Kadhalika, Bashungwa amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Stephen Byabato kwa namna anavyoendelea kusimama kidete kuhakikisha vipaumbele vya Maendeleo katika Jimbo lake Bukoba mjini vinatekelezwa bila kikwazo chochote. 

Awali,  Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa Kagera, Eng. Ntuli Mwaikokesy amesema upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye) - Bukoba Port (kilometa 5.1) utetekelezwa kwa awamu 4. 

Eng. Ntuli amesema Sehemu ya kwanza ya Upanuzi wa njia nne kuanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi eneo la Mitaga utatekelezwa kwa miezi 12 ambapo kazi ilianza Oktoba 9, 2023 na jumla ya Wananchi 25 wamepisha upanuzi wa ujenzi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.8 zitatengwa kulipa fidia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com