Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

𝗧𝗨𝗞𝗢 𝗧𝗔𝗬𝗔𝗥𝗜 𝗞𝗨𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗜𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗦𝗘𝗞𝗧𝗔 𝗕𝗜𝗡𝗔𝗙𝗦𝗜: 𝗲-𝗚𝗔

Na Mwandishi Wetu. 

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imeahidi kushirikiana na Benki ya NMB ili   kuimarisha, kukuza na kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana wa Kitanzania wabunifu na wale wanaosoma fani ya TEHAMA, katika Vyuo Vikuu mbalimbali nchini, kupitia programu maalum ya mafunzo kwa vitendo inayotolewa na e-GA kupitia Kituo chake cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC).

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Benedict Ndomba, wakati wa kikao cha pamoja kati ya e-GA na Benki ya NMB kilichofanyika katika Makao Makuu ya ofisi za e-GA jijini Dodoma, kwa lengo la kujadili namna taasisi hizo zinavyoweza kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya teknolojia.

Maeneo hayo ni pamoja na utafiti, matumizi ya teknolojia za kisasa, kuvumbua vipaji na kuviendelea kwa wavijana wabunifu wa Kitanzania, pamoja na kutoa fursa kwa vijana wavumbuzi na wabunifu ikiwa ni sehemu ya kuendeleza Sekta ya TEHAMA nchini. 

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza na kukuza fursa za ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la TEHAMA, alisema Ndomba .  

“e-GA imekuwa ikishirikiana na Vyuo Vikuu mbalimbali nchini  katika kuwapata vijana wenye ujuzi, hivyo makubaliano hayo kati ya e-GA na NMB ni muendelezo wa ushirikiano mazuri uliopo kati ya e-GA na wadau mbalimbali wa TEHAMA”, alifafanua Ndomba.

Aliongeza kuwa, katika kikao hicho taasisi hizo zimekubaliana kushirikiana na kuandaa mkataba wa makubaliano (MOU) ambapo baada ya kukamilika kwa mkataba huo, pande zote mbili zitakutana na kujadiliana namna ya utekelezaji wa makubaliano hayo. 

“e-GA imekuwa ikiwatengeneza vijana wanaoshiriki programu maalum ya mafunzo kwa vitendo pamoja na utaratibu wa kujitolewa (interns and volunteering) kupitia kituo chetu cha utafiti na ubunifu, kwa kuwajengea uwezo zaidi ili kwenda sambamba na soko la ajira pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoibuka kila siku”, alisema Ndomba.

Aidha, Ndomba aliishukuru Benki ya NMB kwa kuona umuhimu wa kutengeneza wataalamu wazawa wa TEHAMA   kupitia programu hiyo na kuwa,  e-GA ipo tayari kushirikiana na benki nyingine zenye dhamira ya kuijenga Tanzania ya kidijitali katika sekta zote za serikali na binafsi.

Naye Meneja eGovRIDC Dkt. Jaha Mvulla alisema, e-GA ipo tayari kushirikiana na Benki ya NMB katika maeneo mbalimbali yanayolenga kukuza matumizi ya TEHAMA nchini ikiwemo eneo la rasilimali za miundombinu na vifaa vya TEHAMA vya kufanyia mazoezi na majaribio, ubunifu hasa maeneo ya teknolojia mpya, kujenga uwezo na uzoefu kwa vijana, mafunzo kwa vitendo, utafiti na machapisho, maonesho, mashindano mbalimbali ya kidigitali kwa ajili ya kuvumbua vipaji, na maeneo mengine yanayohusiana na jitihada za Serikali Mtandao na teknolojia za kifedha.

“e-GA ipo tayari kufanya kazi na NMB kupitia programu maalumu ya mafunzo kwa vitendo inayoendeshwa na eGovRIDC, ili kuchochea ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya zinazoibuka duniani ikiwemo Akili Bandia (AI), Machine Learning,  Blockchain na matumizi yake kama vile kujenga ulewa wa teknolojia kama za Digital Currency na FinTech, Utengenezaji wa mifumo (System Development) kwa ajili ya kutatua changamoto zetu nchini na usalama mtandaoni (Cyber Security)”, alisema Dkt.Jaha.

Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu- Kituo cha Taaluma NMB Bi. Joanitha Rwegasira alisema kuwa, Benki ya NMB imeandaa programu hiyo ili kuongeza idadi ya vijana wabobezi kwenye masuala ya TEHAMA watakaofanya kazi katika sekta za umma na binafsi kwa lengo la kukuza taifa la kidijitali.

Programu hiyo itasaidia kufanya majaribio ya teknolojia mpya  zinazoibuka ikiwemo Sarafu ya mtandaoni na kutoa suluhu kwenye maeneo mbalimbali yenye changamoto katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwemo matishio ya usalama mtandaoni, ubunifu wa mifumo n.k, alisema Rwegasira

Aidha, aliishukuru Mamlaka kwa kuonyesha utayari wa kushirikiana na NMB na kwamba watatumia fursa hiyo katika kuhakikisha wanaboresha huduma za kibenki hususani huduma zinazotolewa kidijitali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com