Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeitaka Serikali kuongeza msukumo wa fedha kwa wakati ili kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda.
Bwawa hilo linalenga kuwezesha uhai wa kudumu wa mto Ruvu kwa kuhifadhi maji wakati wa masika na hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa siku 365, mikoa hiyo inategemea maji ya mto Ruvu kama chanzo kikuu cha huduma ya maji.
Wito huo umetolewa leo mjini Morogoro kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Felix Kavejuru (Mb) wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa la Kidunda. Amesema mradi huo unaenda kuchochea uchumi wa nchi nzima katika maeneo tofauti tofauti hivyo ni mradi muhimu wa serikali na wenye uzito.
"Huu mradi unaenda kuchochea maendeleo ya Taifa. Tumeambiwa utazalisha umeme megawati 20 ambazo zitasaidia vijiji vinavyozunguka mradi na kuongeza uzalishaji kwenye gridi ya Taifa. Mradi utachochea kilimo, utachochea ufugaji, pia kukuza viwanda. Haya manufaa ni makubwa kwa serikali, wasimamizi na watekelezaji wa mradi wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa viwango vinavyo hitajika" Mhe. Kavejuru amesema.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu fedha zitolewe ili kutekeleza mradi huo. Amesema mradi huo ni wa kimkakati na imekuwa ni ndoto ya Muda mrefu ya Wzara ya Maji kuhakikisha inawezesha upatikanaji wa majisafi kwa wananchi wa mikoa nufaika.
Mhe. Mahundi amepokea maombi ya wananchi wa kijiji cha Mkulazi kupitia Mbunge wa eneo hilo Mhe. Hamis Shaban (Babu Tale) ya kutaka wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi wapewe kipaumbele katika ajira za utekelezaji wa mradi.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa kuhakikisha ndani ya wiki moja anakutana na kufanya kikao na mkandarasi kampuni ya Sinohydro Cooperation Ili kubaini iwapo ajira hizo zinatolewa kwa wananchi husika.
Mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda unatarajia kugharimu shilingi bilioni 329 na unatarajia kukamilika mwaka 2026.