#Aagiza Wakandarasi kukamilisha Mradi kwa wakati
#Wananchi kuondokana na adha ya kukatika kwa Umeme Simiyu
****
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt Yahaya Nawanda amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220 Shinyanga (Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi), pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Simiyu kukamilisha mradi huo haraka ili Wananchi waweze kuondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Dkt. Nawanda ametoa maagizo hayo 25 Oktoba 2023 katika ziara yake katika Wilaya ya Maswa na Bariadi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo.
"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa",amesema Mkuu wa Mkoa Mhe. Dkt. Nawanda.
Aidha Mkuu wa Mkoa Dkt Nawanda ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufikisha umeme katika vijiji 470 ndani ya Mkoa wa Simiyu.
"Katika Nchi hii ni Mkoa wa Simiyu pekee ambao hatumdai Mhe. Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kijiji chochote na kazi yetu tuliyo nayo ni kusafirisha umeme katika Vitongoji baada ya umeme huu kuongezewa Nguvu baada ya kukamilika mradi huu unaotekelezwa wa kusafirisha umeme kV 220",amesema Dkt. Nawanda.
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo Mhandisi Adolf Kigombola amesema tayari kazi za awali zimeanza kutekelezwa na mkandarasi baada ya TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya uhamasishaji kwa Wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali ikichakata malipo ya Fidia.
Aidha ameongeza kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya Fidia kwa waathirika wa mradi na kwamba Wananchi watarajie malipo ya fidia mapema Mwezi Novemba 2023.
Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL)kutoka Nchini India anatekeleza ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220 Shinyanga(Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi),huku kituo cha kupoozea umeme ujenzi wake ukitekelezwa na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD kutoka Nchini China.
Serikali imeelekeza kiasi cha shingi Bilioni 48 kwa ajili ya Utekelezaji wa mradi huo ulioanza utekelezaji wake 10 Machi 2023 ambapo unatarajiwa kukamika ifikapo 9 Septemba 2024.
GCO,
Simiyu RS,
25 Oktoba, 2023
Social Plugin