MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi amemtaka kocha mkuu wa timu ya Geita Gold inayomilikiwa na halmashauri hiyo afike ofisini kwake mara moja kueleza kiini cha matokeo mabaya.
Zahara ametoa maelekezo hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari mjini Geita na kueleza haridhishwi na mwenendo wa timu hivo benchi la ufundi wafike kumueleza kikwazo ni nini.
“Nimetoa wito na angalizo kwa mwalimu wa timu ya Geita Gold Fc, kwanza anione kabla sijamtafuta, yeye pamoja na benchi lake na ufundi, kabla ya hatua yeyote tunaweza tukazungumza, kujua kwamba tunakwama wapi.
“Sisi kama halmashauri wamiliki wa ile timu hatujawajibika wapi, labda tunamkwamisha mwalimu, lakini niwahakikishieni timu ile sisi kama halmashauri tumewajibika kadri ya uwezo wetu kuhakikisha inafanya vizuri.
“Lakini tunataka tuwasikilize na wenzetu wa upande wa pili wanasemaje, kama changamoto itakuwa ni ya kwao tutawapa angalizo la kurekebisha ile changamoto na tunataka tuone matokeo.”
Amekiri matokeo ya suluhu waliyopata Geita Gold Fc ugenini mkoani Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons yanatoa mwanga wa mabadiliko lakini lazima hatua thabiti zichukuliwe kumaliza ukata wa matokeo mazuri.
“Kama changamoto ipo kwa wachezaji basi na kwenyewe tutachukua hatua, hakuna mkubwa zaidi ya mwajiri, na mwajiri ni halmashauri, hakuna mkubwa yeyote kwenye timu zaidi ya mwajiri.
Zahara amesisiza timu ya Geita Gold mpaka sasa ipo kwenye matazamio na yeyeote atakayesumbua na kuonekana kikwazo ndani ya timu atachukuliwa hatua kulingana na makubaliano ya mikataba.
Ikumbukwe Geita Gold Fc inafundishwa na kocha Hemed Suleiman, ambaye tangu apewe dhamana hiyo, imecheza michezo nane ya ligi kuu ya Tanzania bara na kupoteza michezo minne, kupata sare tatu na ushindi mmoja pekee.
Social Plugin