Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma Kanali Michael Majala Ngayalina ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuwafikia wanafunzi 971 wa shule ya Sekondari Buyenzi Kwa lengo la kuwahamasisha wapende masomo ya Sayansi.
Ameyasema hayo alipotembelewa na timu ya uhamasishaji toka DIT inayoendelea na zoezi la uhamasishaji huo kwa shule za Sekondari katika mikoa ya Kigoma, Songwe, Sumbawanga na Mbeya.
"Nashukuru sana kwa kutuchagua sisi Buhigwe ili mzungumze na watoto hawa maana kiukweli wanafunzi wetu wapo nyuma sana kwenye masuala ya TEHAMA na Sayansi kwa hiyo uhamasishaji unahitajika sana japokuwa sisi tunahamasisha lakini wakisikia kutoka kwa wengine itawapa chachu zaidi". amesema Kanali Michael
Kwa upande wake Afisa Elimu Maalum Sekondari, wa Buhigwe Bw. Pius Ndijuye amewataka wanafunzi hao kuzingatia yale waliyoelezwa ili waweze kufaidi fursa zilizopo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi ikiwepo fursa ya kupata ufadhili wa serikali wa kusoma bure chuoni pindi watakapohitimu.
"Niwaambieni ninyi vijana zingatieni haya mliyoelezwa fursa zipo huku kwenye sayansi utasomeshwa bure mzazi hatohangaika lakini pia hata DIT kuja tu kuzungumza nanyi wanafunzi wa Buyenzi ni fursa hivyo muitumie vizuri maana ni kwa manufaa yenu" amesema Ndijuye
Nae msimamizi wa programu ya uhamasishaji kutoka DIT Dkt. Yasinta Manyele ameelezea mafanikiò yaliyopatikana tangu uhamasishaji uanze na kusema kuwa,
"Tulianza uhamasishaji huu kwa kupita kwenye baadhi ya shule za Sekondari huko nyanda za juu kusini, tukapita kanda ya kaskazini pamoja na kanda ya ziwa kwa hayo maeneo machache tuliyoweza kupita imetusaidia kuongeza idadi ya wanafunzi hasa wa kike kwenye masomo ya Sayansi kwa kuwa kabla ya hapo idadi ya wanafunzi wa kike ambao tulikuwa tunawadahili ilikuwa asilimia 21 tu, lakini sasa tumesogea na kufika asilimia 29 kwa hiyo tunasogea."amesema Dkt. Manyele
Aidha Manyele amewataka vijana kuwa na nidhamu kwenye masomo ya Sayansi na ikiwemo kufanya mazoezi ya kile wanachofundishwa kwa bidii binafsi ndiyo itakayowasaidia kufikia ndoto zao.
Hata hivyo zoezi hilo la kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya Sayansi bado linaendelea katika mkoa wa Kigoma.
Social Plugin