WAZIRI KAIRUKI AMWAPISHA KIIZA, KAMISHNA MPYA NGORONGORO


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki leo Oktoba 29,2023 amemwapisha Kamishna mpya wa Hifadhi ya Ngorongoro katika ofisi za makao makuu ya Hifadhi hiyo mkoani Arusha, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Richard Kiiza kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais hivi karibuni.

Akizungumza mara baada ya kumvisha cheo na kumwapisha, Waziri Kairuki amemshukuru Mhe. Rais kwa kufanya uteuzi huo ambapo amesema uteuzi huo ni sehemu ya kuimarisha timu ya utekelezaji wa majukumu ya Uhifadhi, utalii na maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuhudumia watanzania kupitia sekta hiyo na kuhakikisha kuwa wizara inaendelea kuongeza jitihada za kuhifadhi, kutangaza utalii kwa njia mbalimbali za kisasa ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi ya Tanzania.

Aidha amesema Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu zoezi la kuhama kwa hiari kwa wakaazi wa Ngorongoro kuelekea katika maeneo wanayoyachagua huku ikizingatia haki zote za binadamu.

“Serikali inaendelea kuwahakikishia wadau mbalimbali, wananchi wa Ngorongoro na Jumuiya za Kimataifa kuwa zoezi hili ni la hiari, shirikishi na linazingatia misingi ya haki za kibinadamu na utawala bora na kila mwananchi aliejiandikisha kuhama kwa hiari Serikali itampa fidia na gharama zote za kumhamisha hadi alipochagua kwenda zinabebwa na Serikali kwa asilimia 100.” Amefafanua Waziri Kairuki

Ameongeza kuwa Katika awamu hii ya pili ya utekelezaji wa zoezi hili, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari kwa awamu ya pili ikiwemo ujenzi wa Nyumba 5,000 katika Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni, Saunyi Wilaya ya Kilindi na Kitwai Wilaya ya Simanjiro kwa ajili ya kuhakikisha Wananchi walio tayari kuhama wanaandaliwa makazi bora na huduma za kijamii ili waishi Maisha mazuri kama watanzania wengine tofauti na maeneo ya Hifadhi.

Mhe. Kairuki ameonya baadhi ya watu wanaohujumu zoezi hilo na kusisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ambapo pia ameitaka mifugo yote ndani kinyume cha sheria ya Hifadhi kuondolewa.

Kwa upande mwingine Waziri Kairuki amewasisitiza Menejimenti na Watumishi wa NCAA kumpa ushirikiano Kamishna wa Uhifadhi mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambayo amepangiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa malengo ya Shirika ya kuendeleza shughuli za Uhifadhi, kutangaza Utalii pamoja na Maendeleo ya Jamii yanatekelezwa ipasavyo na muda wote, huku akiwataka kuongeza kasi ya utendaji kazi kwa kuwa wabunifu, waadilifu na kujituma zaidi katika kuhudumia watalii na wageni, mbalimbali wanaotembelea Hifadhi hiyo.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mwalimu Raymond Steven Mwangala ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro amempongeza waziri Kairuki kwa kuteuliwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana kikamilifu na Wizara katika kuhifadhi maliasili kwa faida ya vizazi nvya sasa na baadaye.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post