Na. Jacob Kasiri- Kitulo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Benedict Wakulyamba amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa uhifadhi uliotukuka na usio na mashaka kwa taifa.
Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo tarehe 10.10. 2023 alipotembelea Hifadhi ya Taifa Kitulo iliyopo wilayani Makete katika mkoa wa Njombe.
Ndani ya hifadhi hiyo Kamishna Wakulyamba alitembelea Lango la Mwakipembo, Uwanda wa Maua, Maporomoko ya maji ya Mwakilema na Mwakipembo.
Baada ya kuviona vivutio hivyo na baadhi ya mamalia wachache walioonekana kwa muda huo, hakusita kuonesha furaha yake alipotazama upande wa Mashariki na kuona mandhari nzuri iliyonakshiwa kwa safu za milima ya Livingstone na tambarare iliyotaradadi kwa maua yenye rangi tofauti mithili ya zulia.
"Nimeridhishwa na kazi nzuri za uhifadhi mnazozifanya maafisa na askari wa TANAPA. Hongereni kwa kuendelea kuhifadhi rasilimali zetu, serikali na wizara inatambua kazi nzuri mnayoifanya ya uhifadhi kwani mnajituma usiku na mchana.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi mwanamapinduzi kutoka nchini India Mahatma Gandhi aliwahi kusema, Utajiri wa taifa lolote lile duniani unategemeana na jinsi taifa hilo linavyoheshimu na kulinda wanyamapori wake. Hivyo wanachokifanya TANAPA ni kuendeleza falsafa hiyo.
Aidha, Kamishna Wakulyamba alisisitiza maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angela Kairuki (Mb) kutekelezwa, kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege karibu na Hifadhi ya Taifa Kitulo ambao utakuwa chachu ya kukuza utalii na kufungua fursa za uwekezaji kwa wananchi wa maeneo jirani.
" Kufanya kazi kwa uadilifu ndio msisitizo namba moja, msijihusishe na vitendo vinavyokinzana na maadili ya kazi kama vile rushwa na ujangili," aliongeza Kamishna Wakulyamba.
Kamishna Wakulyamba pia, aliwataka maafisa na askari kujiendeleza kielimu alisema, "mnapopata nafasi msisite kujiendeleza katika fani ya uhifadhi au fani nyingine kulingana na matakwa ya taasisi, mnaposoma hakikisheni hamuathiri utendaji kazi wa shirika."
Aidha, Kamishna Wakulyamba alifanikiwa kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Kusini yaliyopo Rujewa Wilayani Mbarali, na kuwapongeza TANAPA kwa ujenzi wa ofisi kubwa na yenye hadhi ya Kanda.
Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Steria Ndaga, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo alisema, "Kanda ya kusini ina jumla ya maafisa na askari 17, kati yao wawili ni wa kike na 15 ni jinsia ya kiume".
"Lengo la uanzishwaji wa kanda hii ni kuratibu na kusimamia shughuli za Uhifadhi, Utalii na mwenendo mzima wa Ikolojia katika Hifadhi za Taifa Ruaha, Kitulo na Katavi" alisema Kamishna Ndaga.
Kanda ya Kusini - TANAPA ilianzishwa mwezi mei, 2019 baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lenye makao makuu yake jijini Arusha kufanya ughatuzi wa madaraka uliopelekea kuanzishwa kwa kanda nne.