Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Shule ya awali na msingi BECO iliyopo manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga imefanya sherehe (mahafali) ya kuwaaga wanafunzi waliohitimu darasa la awali na darasa la saba mwaka 2023.
Sherehe hiyo ya kuwaaga wanafunzi waliohitimu darasa la awali na la saba imefanyika leo Oktoba 6, 2023 katika viwanja vya shule ya awali na msingi BECO.
Akisoma historia fupi ya shule hiyo mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi BECO Mwl. Lucas Mashimba amesema shule hiyo imekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake ambapo mwaka 2021 shule hiyo ilishika nafasi ya 10 kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la saba.
"Shule ya awali na msingi BECO ilianzishwa na kusajiliwa rasmi na serikali mnamo mwaka 2018, kwa kufundisha kwa lugha ya Kiingereza (English Medium), kwasasa shule yetu ina jumla ya wanafunzi 360 wavulana 176 na wasichana 184 na kwenye mahafali haya ya pili ya shule hii tuna wahitimu 14 waliomaliza darasa la saba, 6 wakiwa ni wavulana na 8 wasichana.
Lakini pia tunasheherekea mahafali haya tukiwa na wahitimu wa darasa la awali 30 wasichana 14 na wavulana 16 wanaotarajia kujiunga na darasa la kwanza mwaka ujao", amesema Mwl. Lucas Mashimba.
Kwa upande wake Mdhibiti ubora wa shule Aziza Yanga ameipongeza shule hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma na kuwasihi wazazi na walezi kupeleka watoto kwenye shule zinazotambulika na kusajiliwa ili kujihakikishia elimu bora inayotolewa kwa watoto wao.
"Palipo na dosari sisi kama wadhibiti ubora wa shule hatupepesi macho lengo ni kujenga kizazi chenye elimu bora na si bora elimu, wakazi wa Shinyanga tujivunie kwamba BECO PRE & PRIMARY SCHOOL ni miongoni mwa shule bora hapa nchini", amesema Aziza Yanga.
Mkurugenzi wa shule hiyo Machiya Ngelela ameeleza malengo na kipaumbele kikubwa cha shule hiyo kuwa ni taaluma bora hivyo anawakaribisha wazazi na walezi kupeleka watoto wao katika shule ya hiyo ili waweze kupata elimu bora itakayowavusha kwenda ngazi nyingine kitaaluma.
Akizungumza kwa niaba ya aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Katibu Tawala wilaya ya shinyanga Said Kitinga amewasihi wazazi kuendelea kuzingatia malezi kwa watoto wao pindi wawapo nyumbani na kuwasihi wazazi wengine kupeleka watoto shuleni hapo ili wapate elimu bora katika shule ya msingi na awali BECO.
"Kwa kutambua mchango wa taasisi binafsi kwenye sekta ya
elimu, kwa uwepo wa shule ya awali na msingi BECO hapa Shinyanga inayokidhi
vigezo vya ufundishaji, wazazi naamini bado chaguo lenu ni shule ya BECO Pre
& Primary School kulingana na mazingira pamoja ubora wa elimu inayotolewa
katika shule hii kupitia waalimu na uongozi wa shule hii", amesema Said
Kitinga.
"Mara baada ya watoto hawa kumaliza elimu ya darasa la saba
wawapo nyumbani tuendelee kuwafundisha kwa kusimamia maadili na miiko
yetu, lakini pia tuendelee kutoa taarifa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi
na usalama ili kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto", ameongeza Said
Kitinga.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akiwa kwenye mahafali hayo
Mwalimu Mkuu wa shule ya awali na msingi BECO Mwl. Lucas Mashimba akisoma taarifa fupi ya Shule hiyo.
Mkurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi BECO , Machiya Ngelela akizungumza wakati wa mahafali ya shule hiyo.
Mthibiti Ubora wa Shule Aziza Yanga akizungumza wakati wa mahafali hayo.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga Akizungumza wakati wa Mahafali ya shule hiyo
TAZAMA PICHA MBALIMBALI
Baadhi ya wazazi na walezi walioudhulia kwenye mahafali ya shule hiyo.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akikabidhi vyeti kwa wanafunzi waliohitimu shuleni hapo,
Picha ya pamoja.