Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MANISPAA YA TABORA YAINGIA MKATABA WA MIAKA 33 NA BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA


Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imeingia Mkataba wa miaka thelathini na tatu (33) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuwapa jengo mojawapo ya majengo yake ili Benki hii iweze kutoa huduma kwa wakulima wa Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi, na kwa mujibu wa makubaliano hayo Benki itatakiwa kurudisha jengo hilo baada ya muda huo kuisha.

Mkataba huu umetiwa saini leo Oktoba 27,2023 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora ambapo kimsingi umeanza kutekelezeka tangu tarehe 17/06/2022.

Ndugu Elias M. Kayandabila ametia saini kwa niaba ya Manispaa ya Tabora akishuhudiwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe.Rose Kilimba pamoja na Mwanasheria wa Manispaa Ndugu Robert Matungwa.

Dkt.Kaanaeli Nnko ambae ni Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ametia Saini kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Ndugu Frank Nyabundege huku Mkuu wa Idara ya Sheria ya Benki hiyo Dkt. Edson Lwechungura akishuhudia makubaliano haya.

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kwa vitendo kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo kwa kutambua mchango mkubwa wa Sekta hii katika pato la Taifa na kwa Mwananchi mmoja mmoja, hivyo pamoja na kuweka ruzuku kubwa kwenye mbolea bado inaona kuna umuhimu mkubwa angalau kila Kanda iwe na Benki ya Kilimo kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima huduma zingine kama mikopo ya kilimo yenye liba nafuu.

Kwa mantiki hii basi, Manispaa ya Tabora imeunga mkono jitihada za Serikali kwa vitendo kwa kutoa jengo lake ili wakulima wa mikoa hii ya kanda ya Magharibi iweze kupata huduma zitakazotolewa na Benki hii , ambapo ni matarajio kuwa hadi muda huu wa makubaliano kufika ukomo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania itakuwa imeshapata jengo lake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com