Wanawake mkoani Shinyanga wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupata PHD ya heshima huko Nchini India na kuleta Fedha nyingi za kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta ya afya,elimu maji na nishati ya umeme.
Kongamano hilo la kumpongeza Dkt. Samia limefanyika leo Oktoba ,12,2023 Manispaa ya Shinyanga likiongozwa na mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme na kuhudhuriwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Mabala Mlolwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed.
Mndeme amewaeleza wanawake hao kuwa Serikali ya awamu ya sita imeleta Fedha nyingi za maendeleo na kila Kijiji kimefikiwa na mradi ambapo sekta ya elimu Serikali imeleta zaidi ya sh Bilioni 53.6 ikiwa shule mpya 24 zimeongezeka,maabara 57 kwa shule za sekondari na nyumba za walimu 69.
Mndeme amesema kwa upande wa nishati ya Umeme Serikali imeleta zaidi ya sh Bilioni 323 kwa ajili ya mradi mkubwa wa nishati ya Umeme jua unao tekelezwa kwenye Kijiji cha Talagha wilayani Kishapu ambao utakuwa ni mradi mkubwa kwa Afrika Mashariki .
"Umeme jua utatarajia kutoa Megawati 150 na kuondokana na changamoto ya wananchi kukosa Umeme kwa tatizo la kukatikakatika",amesema Mndeme.
Mndeme ameongeza kuwa katika sekta ya Afya hospitali zilikuwa nane na sasa zimeongezeka mbili na kufikia hospitali kumi ambapo hospitali ya halmashauri Ushetu na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga zimeanza kufanya kazi na Vituo vya afya vimeongezeka sita na kufikia 25 na Zahanati kumi na moja zimeongezeka na kufikia Zahanati 242.
Serikali imeleta zaidi ya sh Bilioni 102 na kutekeleza miradi ya maji 47 sawa na ongezeko la miradi 15 huku miradi mipya 66 ikianzishwa katika vijiji mbalimbali kwa lengo la kumtua ndoo mama kichwani.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza kwenye kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu
Viongozi wanawake wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa akizungumza kwenye kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan
Wanawake wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa akizungumza kwenye kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu