Na Mwandishi maalum..
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Tarehe 8 Oktoba, 2023 amewasha kwa mara ya kwanza umeme kwenye kijiji cha Litumbandyosi, Kata ya Litumbandyosi kwenye Halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Mhe. Judith Kapinga amesema, umeme ambao umefika kwa mara ya kwanza katika kijiji hicho ni haki ya Wananchi hao kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilitenga fedha kwa muda mrefu na kuwataka Wananchi hao kuchangamkia fursa ya kujiunga na huduma hiyo ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Wananchi wa Litumbandyosi ni haki yenu kupata umeme na Serikali ilishatenga fedha kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu na Mzunguko wa Pili chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA); fursa hii, ilitengewa fedha, zaidi ya mwaka mmoja ulilopita”. Alisema Mhe. Judith Kapinga.
Ameendelea kusema kuwa, Mhe. Rais ametoa fedha kwa vijiji vyote vya Tanzania ambavyo bado havijapata umeme, ili vipate umeme ikiwemo vijiji vinne (4) vya Kata ya Litumbandyosi vilivyopo katika wilaya ya Mbinga na kuongeza kuwa jumla ya shilingi bilioni 2.07 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Mhe. Kapinga amesema kuwa Serikali, itapeleka umeme katika maeneo yote, yenye shughuli za kijamii na kiuchumi, zikiwemo taasisi kama shule, vituo vya afya, misikiti, na makanisa.
Katika taarifa yake ya awali kwa Naibu Waziri; Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Yusuph Ismail ambaye pia ni Meneja Tathmini na Ufuatiliaji wa Miradi REA amesema mkoa wa Ruvuma, REA ilitenga jumla ya shilingi bilioni 91.2 kwa ajili ya Miradi yote ya kupeleka nishati ya umeme vijijini kati ya fedha hizo, Wilaya ya Mbinga imepewa shilingi bilioni 28.8 kwa ajili ya Miradi hiyo ambapo kwa Kata ya Litumbandyosi na kijiji cha Litumbandyosi pekee yake Mkandarasi Kampuni ya NAMIS Corporate LTD ametumia shilingi milioni 971 kukamilisha Mradi huo ambao Naibu Waziri ameuwasha.
Mhandisi, Ismaili ameongeza kuwa katika fedha hizo Mbinga vijijini imepata shilingi bilioni 19.8 na Mbinga mjini imepata shilingi bilioni 9.
“Kwa upande wa Mbinga vijijini, Mkandarasi anatarajia kupeleka umeme vijiji 45 vilivyobaki hdi kufikia Desemba 30, 2023” amesema Mhandisi Ismail.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewaahidi Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambao vijiji vyao bado havijafikiwa na huduma ya umeme kwamba watahakikisha vijiji hivyo, vinapata umeme kabla ya mwezi Desemba 30, 2023.
“Mhe. Rais ametoa fedha mpate umeme, mtapata umeme. Niwahakikishie ndugu zangu wa Kingoli, umeme unakuja, tutamsimamia Mkandarasi kuhakikisha nguzo zinakuja na umeme unawasha, ili na ninyi pia mpate umeme. Hatutawaangusha, tutahakikisha mnapata umeme,” amesema Naibu Waziri, Kapinga.
Naibu Waziri Kapinga alimuita Mhandisi, Shaidu Rutakolezibwa, Meneja Miradi kutoka kampuni ya NAMIS Corporate Ltd (Mkandarasi) anatekeleza mradi huo wilaya ya Mbinga kuja mbele ya Wananchi na kusema ni lini atakamilisha kazi ya kufikisha umeme kwa Wananchi hao ambapo, Meneja huyo aliahidi kukamilisha viijiji 45 vya Mbinga vijijini kabla ya Desemba 30, 2023.