Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ONESHO LA KIMATAIFA LA SITE 2023, KUPAMBWA NA WANYAMA HAI



Na John Mapepele.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa maandalizi ya Onesho la saba la Utalii la Kimataifa la Swahili International Tourism Expo – S!TE 2023 yamekamilika ambapo kwa mara ya kwanza kutakuwa na bustani ya wanyama hai.
Akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari leo Oktoba 3, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam amesema onesho hilo litafanyika kuanzia Oktoba 6 - 8 mwaka huu ambapo wageni na wadau muhimu wa sekta kutoka maeneo mbalimbali duniani watahudhuria.


“Katika kipindi chote onesho hili limekuwa jukwaa muhimu na lenye ushawishi kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi walio katika mnyororo wa huduma za utalii.” Amefafanua Mhe. Kairuki.

Waziri Kairuki amewataja baadhi ya wadau watakaoshiriki kwenye maonesho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na Mabalozi wa nchi mbalimbali, Bodi za Utalii kutoka nchi za Afrika zikiwemo Uganda na Malawi, Waoneshaji (Exhibitors) zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya nchi. Wanunuzi wa biashara za utalii (Buyers) zaidi ya 70 kutoka katika masoko yetu ya Kimkakati ya kimataifa hususan, Ulaya, Amerika na Asia.


Aidha, amesema onesho la mwaka huu litapambwa na Bustani ya Wanyamapori hai ili kuwavutia watembeleaji (visitors) na kuhamasisha Utalii wa ndani, pamoja na Jukwaa la Uwekezaji la Utalii (Tanzania Tourism Investment Forum-TTIF) na ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuja kutembelea na kuona hazina na urithi wa utalii wa Tanzania pia


“Natoa rai kwa watanzania, wawekezaji, na wadau wengine wa utalii kushiriki kikamilifu onesho la SITE 2023, ambalo ni fursa ya muhimu kukutana na wadau wenzenu waliopo katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Utalii, ili kwa pamoja tuhakikishe sekta hii inapiga hatua tukitambua melengo makubwa tuliyonayo ya kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Halikadhalika kuendelea kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia utambulisho wetu wa Tanzania, Unforgettable na Programu ya Tanzania – The Royal Tour.” Amesisitiza Mhe. Kairuki.


Waziri Kairuki ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea mtandao wa site.tanzaniatourism.go.tz ili kuona mambo muhimu yanayohusu onesho hili ikiwa ni pamoja na semina mbalimbali, midahalo inayoangazia mada za utalii na fursa za uwekezaji ambapo amesema Kauli mbiu ya Onesho la S!TE 2023 ni: Utalii Unaowajibika kwa Maendeleo Jumuishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com