Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. MKENDA: VYUO VIKUU VIJIKITE KWENYE TAFITI ILI KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametoa wito kwa vyuo vikuu kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija nchini ili kuchochea na kuleta ushindani katika gunduzi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Prof. Mkenda, ametoa wito huo leo Oktoba 9, 2023, wakati akilizindua baraza jipya la chuo Kikuu Huria cha Tanzania la 2023/2026 katika kituo cha chuo hicho mkoa wa Dodoma kilichopo jijini Dodoma.

“Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na wingi wa mapato, kuna vipengele vingi vya upimaji ubora wa elimu ya chuo kikuu mojawapo ni ufanyaji wa tafiti zenye kuleta gunduzi, kukuza maarifa na ujuzi katika jamii. Lazima chuo kikuu kiwe chemchem ya kuvumbua na kutafuta majibu ya kutatua matatizo ya wanachi kwa kufanya tafiti na kuja na majawabu. Chuo Kikuu ni mahali pa kuzalisha wataalamu na wabobezi ambao wakitoka wanakwenda kufanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali.” Amesema Prof. Mkenda.

Aidha, aliendelea kusema kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vyetu ni vyema zikashindanishwa kimataifa ili ziweze kuwa na viwango vya ubora zaidi katika nyanja za kimataifa ili kuvifanya vyuo vyetu viwe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa mataifa mbalimbali duniani. Ameeleza kwamba hivi karibuni wizara imetoa tuzo na fedha kwa watafiti ambao wamechapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa kama motisha lakini pia kuwafanya watafiti wa Tanzania kushindana kimataifa. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepongezwa kwa kazi nzuri ya kuendelea kuzalisha wataalamu na pia kufanya tafiti mbalimbali ambapo katika tuzo hizo mhadhiri mmoja kutoka Chuoni hapo alipata tuzo hizo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Joseph Kuzilwa, amemuhakikishia mhe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa baraza jipya lililoteuliwa ni la watu wenye taaluma na ujuzi wa kutosha kuweza kulisongesha mbele gurudumu la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

“Timu hii ya wajumbe itakuwa ni chachu kubwa katika kuchangia ufanisi wa baraza kwenye kusimamia chuo kwa mujibu wa majukumu yaliyoainishwa katika hati idhini ya chuo ya mwaka 2007, sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005 na waraka namba moja wa msajili wa hazina wa mwaka 2023. Ufanisi katika usimamiaji wa mpango mkakati mpya wa chuo wa miaka mitatu 2023/24 hadi 2025/26 itakuwa ni moja ya kipimo cha baraza hili kwa kipindi chake cha miaka mitatu.” Amesema Prof. Kuzilwa.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema baraza hili jipya limepata fursa ya kupata mafunzo ya siku tatu ambapo wawezeshaji watatoa mada mbalimbali zitakazowawezesha wajumbe kujenga uwezo zaidi ili waweze kufanya kazi na kutimiza wajibu wao vizuri.

“Utendaji wa baraza hili utapimwa na ofisi ya msajili wa hazina kila mwisho wa mwaka, ndiyo maana tumekaa pamoja ili wajumbe waweze kujua vizuri wajibu, taratibu, haki na mamlaka waliyonayo ili waweze kufanya kazi kwa kukidhi matakwa ya sheria na kanuni zilizopo kuhusu utendaji wa bodi na mabaraza yaliyoko chini ya serikali.” Amesema Prof. Bisanda.

Akitoa historia ya Baraza hilo, Mwanasheria wa Chuo ambaye pia ni Katibu wa Baraza Wakili Nelly Moshi, amesema baraza hili lilianzishwa rasmi mwaka 1994 chini ya uenyekiti wa hayati Basil Mramba kama mwanzilishi na kufuatiwa na wenyeviti wengine kadhaa na mwaka 2022 chuo kiliweza kumpata Mwenyekiti wa sasa Prof. Joseph Kuzilwa kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wajumbe wa Baraza jipya la chuo wanaendelea na mafunzo mpaka tarehe Oktoba 11, 2023 katika kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoa wa Dodoma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com