Na mwandishi wetu.
Jumla ya vijana 6,000 kutoka Shirika la Suma JKT la Jeshi la Wananchi Tanzania,(JWTZ) wameanza kuwasili wilayani Handeni mkoani Tanga kwaajili ya shughuli ya ujenzi wa nyumba 5,000 katika kijiji cha Msomera.
Akizungumzia kuhusu ujio wa vijana hao, wilayani Handeni,Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa,(JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema shughuli yao itakuwa ni ujenzi wa nyumba hizo na tayari Vijana 500 wamesharipoti kwenye mradi na wengine wanaendelea kuingia.
Amesema tayari wameshapokea fedha kutoka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro,kwaajili ya kujenga nyumba hizo ambapo muda wa ujenzi utakuwa ni miezi sita kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi 2024
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro Jenerali Venance Mabeyo kwa upande wake amezitaka wizara za kisekta,kuharakisha ujenzi wa miundombinu katika eneo la mradi kijiji cha Msomera ili wahusika waweze kuanza kazi.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando amesema wanatarajia kusimamia ujenzi huo kwa wakati,ili kuepukana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa mvua ambayo inaweza kuleta changamoto katika kusafirisha vifaa vya ujenzi.
Jumla ya Shilingi bilioni 97 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa nyumba hizo 5000,kwa ajili ya wananchi watakaohama kwa hiari kutoka eneo la Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro.