Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAASISI YA MWALIMU NYERERE KUZINDUA MRADI WA KITAIFA WA MAADILI NA UZALENDO




Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Joseph Butiku alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Babati Mkoani Manyara.

Na. Jawadu Kinyobwa, Babati + Manyara

Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) inatarajia kuzindua mradi wa Kitaifa wa Maadili na uzalendo Oktoba 14, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mkoani Manyara unaolenga kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Joseph Butiku Oktoba 9, 2023 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Babati Mkoani Manyara.

Amesema kwa mujibu wa Tafiti zilizofanyika hivi karibuni, zimebainisha kuporomoka kwa maadili na uzalendo hali inayo pelekea vitendo viovu katika jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia, wizi, ulevi na matendo mengine ambayo ni kunyume na maadili ya kitanzania.

Butiku amesema ustawi wa Taifa lolote unahitaji Amani, Umoja na Maendeleo ya watu wake na nguzo kuu ya mambo hayo ni imani na maisha yanayozingatia usawa wa binadamu wote na haki sawa kwa wote.

“Amani ndio msingi wa kila jambo, Amani ni msingi wa umoja na maendeleo ya ustawi bora wa Taifa. Umoja ni nguvu, umoja ni uzalendo, Hakuna lolote kubwa linaloweza kufanyika bila umoja au kushikamana kwa jamii husika, iwe ndogo au kubwa, kabila au Taifa” amesema Butiku

Aidha, amesema kumomonyoka kwa maadili ya watanzania kunasababishwa na uwepo wa mitandao ya kijamii inayoruhusu upatikanaji wa habari ambazo hazina manufaa kwa Taifa na changamoto za Maisha zinazo wasahaurisha wazazi na walezi malezi bora ya watoto wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com