Na Mwandishi wetu,Dar Es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Austria zimekubaliana kwa pamoja kuimarisha sekta za elimu ya ufundi pamoja na utalii ili kufikia malengo ya Serikali katika katika kuutangaza utalii.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika Mkutano wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki (Mb) na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki amesema kuwa wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kilimo, elimu ya ufundi ambapo Tanzania kwa sasa msukumo wake ni elimu ya ufundi na tayari serikali imeanza kuboresha sera ya elimu na mitaala ya elimu.
“Austria wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika masuala ya tasnia ya ukarimu na utalii, wenzetu kwa mwaka wanapata watalii takriban milioni 40 na wamepiga hatua kubwa, nimefurahishwa pia kuona katika ujumbe alioambatana nao Prof. Kocher kuna wafanyabiashara na wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya utalii, uwekezaji wa hoteli na mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya utalii alisema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, wamekubaliana kushirikiana katika sekta za afya, pamoja na sekta binafsi nchini kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni salama na rafiki.
Naye Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher amesema Austria itaendeleaa kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali hususan miundombinu, kilimo, usindikaji wa chakula, elimu ya ufundi, afya, ajira/kazi, nishati pamoja na utalii kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tanzania kufungua Ubalozi wake nchini Austria, umetuwezesha kushirikiana katika sekta mbalimbali mathalan sekta ya elimu ya ufundi pamoja na utalii,” alisema Prof. Kocher
Prof. Kocher aliongeza kuwa asilimia 40 ya vijana nchini Austria wamekuwa wakipatiwa elimu ya ufundi katika fani tofautitofauti, hivyo Austria inaamini kuwa endapo watashirikiana na Tanzania kuwapatia vijana elimu ya ufundi itasaidia kuwawezesha kupata fani mbalimbali zitakazo wasaidia kujenga Maisha yao na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.
Akiongelea kuhusu sekta ya utalii, Prof. Kocher amesema kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha kuwa Austria na Tanzania zinakuwa na utalii endelevu pamoja na kuhakikisha kuwa mataifa hayo yanakuwa na vivutio bora vya utalii kwa miongo ijayo.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Austria kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mhe. Waziri Kocher yupo nchini Tanzania kwa ziara yake ya kikazi ya siku moja na ameambatana na ujumbe wa wawekezaji 20 kutoka Austria wanaolenga kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za utalii, afya, nishati, elimu, ujenzi na miundombinu.
Tags:
habari