Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YATOA ELIMU KWA WANANCHI 5615


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa Elimu kwa umma katika Halmashauri ya wilaya za Igunga , Kaliua, Sikonge, Uyui na Manispaa ya Tabora mkoani Tabora juu ya umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa, kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo, sambamba na kuwahamasisha wajasiriamali wadogo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.

Kampeni hiyo ya Elimu kwa umma imefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Sokoni, Stendi, Minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo Ubora wa Bidhaa.

Bw.Gibson Milambo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kaliua aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi na alishauri kufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara madukani hususani katika bidhaa za chakula na vipodozi katika ngazi za wilaya.

Akizungumza wakati wa Kampeni hiyo, Meneja Wa Uhusiano na Masoko TBS Bi. Gladness Kaseka amesema lengo la Shirika hilo ni kutoa Elimu Kwa Umma katika Ngazi za Wilaya zote na mpaka sasa Shirika limeshafikia wilaya 72.

Wananchi wamelipongeza Shirika la Viwango Tanzania Kwa Elimu waliyoamua kutoa kwa maana itawasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kununua bidhaa.

Kwa upande wake Mkaguzi (TBS) Bw. Magesa Mwizarubi amewasisitiza wajasiriamali na wafanyabishara kuhakikisha wanauza bidhaa zilizothibitishwa ubora wake na TBS na wenye majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi kuyasajili ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Magesa aliwafafanulia wananchi umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku na kuwaasa wawe mabalozi wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi sambamba na kutoa taarifa katika ofisi ya TBS zilizopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano yaliyotolewa iwapo watakutana na changamoto zihusuyo masuala ya ubora wa bidhaa wakati wa manunuzi.

Kampeni hii imeweza kuwafikia wananchi 5615 kati yao wajasiriamali ni 215 na wananchi 5400,"

Kampeni ya kuelimisha umma ni endelevu na itaendelea katika wilaya za mkoa wa Mtwara na Lindi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com