Meneja Viwango wa TBS Bw. Yona Afrika akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18,2023 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam
********************
Na Grace Semfuko, MAELEZO
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limewataka wauzaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya magari, pamoja na wafungaji wa mifumo na vifaa vinavyohusika na usambazaji wa gesi hiyo, kuzingatia ubora wa viwango vinavyohitajika, ili kulinda afya za watumiaji wa bidhaa hiyo.
Aidha Shirika hilo pia limepiga marufuku uagizaji wa mitungi ya mtumba ya gesi hiyo ya magari, ambayo inatumika kama mbadala wa mafuta kutokana na kuwa na ukomo wa matumizi yake.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Meneja Viwango wa TBS Bw. Yona Afrika amesema shirika hilo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali, limeratibu uandaaji wa viwango vyavituo vya kujazia gesi na vifaa vinavyotumika kwenye mfumo wa gesi za kwenye magari pamoja na karakana ambazo zinafanya shughuli za kubadilisha mitungi.
“Hii mitungi kutokana na mshindilio mkubwa huwa ina kikomo cha matumizi, mingine inatumika mpaka miaka 20, mingine miaka 30, lakini mzalishaji anatakiwa awe ameandika, na kutokana na kwamba hii sekta hapa nchini kwetu ningeni kidogo, na takwa la kikomo cha matumizi ya hii mitungi, kwa sasa tumekataza kuingizwa kwa mitungi iliyotumika kwa sababu hatuwezi kujua imetumika kwa kiasi gani kabla haijafika nchini, kwa hiyo kwa sasa hivi haturuhusu kuingiza mitungi ambayo imetumika, tunaruhusu tu le ambayo ni mipya” amesema Bw. Afrika.
Amesema mpaka sasa hakuna athari yoyote iliyojitokeza kutokana na kubadilisha mifumo ya gesi za magari kutoka kwenye mifumo ya mafuta iliyokuwa ikitumika awali.
“Kwa viwango ambavyo tumeviweka mpaka sasa, hakuna athari za mabadiliko kutoka kwenye mfumo wa mafuta wa kawaida ambao gari lilitengenezwa nao kwenda kwenye mfumo wa gesi asilia ya mgandamizo, kwenye suala la ubadilishaji wa magari kuna hatua ambazo zinadhibitiwa na taasisi mbalimbali, hatua ya kwanza ni kuangalia ubora wa vifaa vinavyotumika kwenye kubadilisha mifumo ya gesi, ambavyo vingi vinatoka nje ya nchi na jukumu hili ni la TBS” amesema Bw. Afrika.
Nae Afisa Viwango wa TBS Bw. Anold Mato amesema mitungi ya gesi asilia inayotumika kwenye magari kama isipodhibitiwa ipasavyo inaweza kuleta madhara kwani mdandamizi wake wakati wa kujaza gesi hiyo ni mkubwa.
“Haya matumizi ya gesi kwenye magari ili kuweza kupata gesi ya kuweza kutembea umbali wa kutosha, inatakiwa gesi iwe imeshindiliwa sana, na kutokana kushindiliwa kwa presha hiyo, kunaweza kutokea kwa hatari endapo mtungi utapasuka au kutokea kwa ajali ya aina yoyote, hapa tunaweka msisitizo mkubwa sana kwenye udhibiti wa hivi vifaa lakini jicho letu lipo kwenye huu mtungi zaidi, kwa sababu ndio kifaa ambacho kinahitaji umakini mkubwa kwenye udhibiti, na kuhakikisha huu mfumo unakuwa salama” amesema Bw. Mato.
Amesema matakwa ya viwango vya mitungi ipo ya aina mbalimbali na ya ujazo wa aina tofauti, na ya malighafi tofauti huku akizitaja aina hizo kuwa ni pamoja na mitungi ya chuma moja pekee, mitungi ya chuma ambayo imetengenezwa kwa kuchanganywa na malighafi zingine, na mitungi ambayo haina chuma kabisa, na aina zote zinakubalika.
Meneja Viwango wa TBS Bw. Yona Afrika akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18,2023 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam
Afisa Viwango wa TBS Bw. Anold Mato akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18,2023 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam
Social Plugin