19 Oktoba 2023
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, kwa kupitia programu yake ya “Our rights, Our Lives, Our future” inayofahamika kama O3 kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania kupitia TBC FM, limeendesha mafunzo yanayolenga kuimarisha uwezo wa waandishi wa redio jamii kutengeneza vipindi vya redio vinavyotoa elimu kuhusu afya ya uzazi,Mimba za mapema/zisizotarajiwa, Ukatili wa kijinsia, VVU/UKIMWI, na Haki ya Elimu kwa watoto hususani watoto wa kike wanaopata ujauzito angali wapo shuleni kwa waandishi radio jamii.
Mafunzo haya yanatolewa jijini Dodoma kwa waandishi 42 kutoka radio jamii za mikoa zaidi ya 11 ikiwemo Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Kigoma, Iringa,Tabora, Arusha, Tanga, Dodoma, Pemba na Unguja kuanzia tarehe 17 hadi 20 Oktoba 2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya mafunzo haya inatokana na mchezo wa tamthilia wa radio (radio drama series) ujulikanao kama “Let’sTalk EUP” yaani “Hebu Tuzungumze kuhusu Mimba za mapema na zisizo tarajiwa”, mchezo ambao hapo awali ulirushwa na radio ya taifa (TBC FM) kutoka Septemba hadi Desembea 2022. Wakati walengwa wakuu wa tamthilia hii wakiwa ni Vijana, “Let’s Talk” inazungumza pia na Wazazi, Walimu, viongozi wa dini, na Jamii nzima kwa ujumla na nafasi zao katika kuhakikisha vijana wana afya bora na ustawi katika kukamilisha safari yao ya masomo bila vikwazo.
Ikiwa ni sehemu ya kufikia jamii zilizopo pembezoni, kwasasa UNESCO inasapoti kutoa elimu kwa radio jamii ili kuweza kurusha tamthilia hii kwenye vipindi walivyonavyo tayari kwa ngazi ya jamii , radio zinazoshiriki ni pamoja na Loliondo FM, Huheso FM, Uyui FM, , Karagwe FM, Mazingira FM, Dodoma FM, Uvinza FM, Micheweni FM, Triple A FM, Tumbatu FM, Joy FM, Radio Fadhila, na radio za vyuo vikuu ikiweo Hope FM ya Chuo kikuu cha Iringa na Saut FM ya chuo kikuu cha SAUT Mwanza.
“Lengo letu ni kusaidia juhudi za serikali kupitia wadau mbalimbali ikiwemo redio jamii ili vijana walio na wasio shuleni wapate elimu sahihi inayozingatia mila na desturi kuhusu afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia, VVU/UKIMWI na Haki ya kupata Elimu” – Mathias Luhanya, Mratibu wa Programu za Afya na Ustawi - UNESO
Mbali na program ya kutoa elimu kupitia redio, mradi wa O3 unasapoti programu mbalimbali za vijana ikiwemo uanzishwaji na usimamizi wa madawati ya jinsia vyuoni (14), mafunzo endelevu kwa walimu juu ya stadi za maisha, utoaji wa Elimu rika (Providers-led Peer Assisted Program), utoaji wa kozi mtandao ihusuyo elimu ya kina ya stadi za maisha zinazozingatia VVU/UKIMWI, Afya ya uzazi na jinsia (CSE), Uboreshwaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya kwa vijana vyuoni, pamoja na utoaji wa mafunzo kwa watoa huduma za afya juu ya utoaji wa huduma rafiki za afya kwa vijana.
Social Plugin