Na Beatus Maganja
Wanyamapori hai wametajwa kuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya Utalii Mwana Katavi yanayofanyika wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi kiasi cha kufanya wakazi wa Mkoa huo kufurika katika banda la TAWA ili kupata maelezo kuhusu tabia na fursa za ufugaji wa Wanyamapori hao.
Maonesho haya ambayo hufanyika Kila mwaka Mkoani humo yalifunguliwa rasmi Oktoba 25, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko ambapo leo Oktoba 31, 2023 yanatarajiwa kufikia tamati.
TAWA imeshiriki na kutumia maonesho hayo kuhamasisha utalii wa ndani kwa kuwahimiza wakazi wa Mkoa huo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo ukanda wa magharibi hususani bustani ya Wanyamapori hai Tabora almaarufu Tabora ZOO iliyo chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
Wanyamapori waliokuwa kivutio katika maonesho hayo ni Simba, chui, fisi, Kobe na ndege wa aina mbalimbali ambao walichochea udadisi wa uelewa kwa wanafunzi wa shule za awali na sekondari waliotembelea banda la TAWA
TAWA inaendelea kutumia vyema maonesho mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi yetu kunadi fursa za utalii na uwekezaji zilizosheheni katika taasisi hii ili kuchangia katika lengo la Serikali kufikisha idadi ya watalii Millioni Tano (5) ifikapo 2025