Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATAALAM NGAZI YA KATA WATAKIWA KUWA NA MPANGO KAZI WA KUPIMA UTEKELEZAJI WA MAENDELEO



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na makundi maalum Wakili Amon Mpanju amefungua mafunzo ya mpango wa Taifa wa kuhamasisha na kusimamia maendeleo ngazi ya msingi kwa wataalamu wa ngazi ya kata Jijini hapa huku akiwatwisha mzigo  wa mambo makuu manne ikiwemo kuwashirikisha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo leo Oktoba 5,2023 Jijini hapa ameeleza kuwa  Viongozi wataalamu ngazi ya kata wanatakiwa kuhakikisha wanaweka mpango kazi unaopimika wa utekelezaji maendeleo ngazi ya masingi kwenye maeneo yao ili kuakisi  maudhui ya mpango huo wa kitaifa unaosimamia maendeleo.

Amesema Mafunzo hayo yana lengo la kuhamasisha maendeleo ngazi ya msingi na kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizoko kwenye maeneo yao utafanikiwa ikiwa watatoka ofisini kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwa wakati.

“Nawasihi mkawajibike kwa kufanya kazi zenye matokeo  kwa kuzingatia umoja na uzalendo kwa kushirikishana ngazi na kata kuheshimiana kwa taaluma mshirikishane ujuzi na maarifa mchape kazi kama timu ndo mtaweza kufikia nia ya watanzania kuwa kitovu cha maendeleo ngazi ya msingi,’’amesema.

Mpanju  ameelekeza kuwa mpango kazi huo ufanyike na kila mtu kwenye eneo lake kwa kuwasilisha taarifa ya kina ya uwajibikaji wake namna anavyowahudumia wananchi ili kufanya tathmini kwa pamoja na kuweka mkakati wa maboresho ya kiutendaji.

Amesema,’’Mkiyaishi hayo tutakuwa na matokeo tarajiwa,mkahakikishe wananchi wanatoa ushirikiano ,muelewe huu mpango ni muhimu kwa Serikali hivyo mkautekeleze kwa vitendo,Kumbukeni Serikali imewagharamia mje mjifunze ili kuwaelimisha wananchi na kuwa na maendeleo ya pamoja ngazi ya msingi na taifa kwa ujumla,”ameeleza

Mbali na hayo amewataka washiriki hao kuwa makini na mijadala inayoendelea kwenye mafunzo hayo huku akiwatahadharisha  kuachaa na matumizi ya simu bila mpangilio ili kuondoka na mkakati mmoja wa kuleta mapinduzi ya fikra na kuwafanya wananchi wajitambue.

“Tunafahamu kwa muda mrefu sasa,utendaji wa ngazi ya msingi umekuwa hauleti tija inayotakiwa kutokana na uzembe wa kitaalam,hakikisheni mnabadilisha utaratibu wa kufanya kazi wasikilizeni wananchi wanataka nini kwa sababu ninyi ndio mabalozi wa Serikali hivyo mkahakikishe mnakuwa mabalozi wazuri katika kuisemea serikali wakati wote,” amesisitiza

Kwa upande wake Mkurugenzi wa maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amewaelekeza wataalam hao kutumia nafasi hiyo kujifunza namna ya kuwahudumia wananchi ili kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

Amesema,”wananchi wanapenda huduma bora,na huduma hiyo inatokana na ninyi kuwa watendaji wazuri,wakiipenda huduma inamaanisha wanaipenda serikali yao, wakiichukia Serikali ni sisi ndiyo sababu,ili kufanikiwa lazima uzalendo na maadili yakawe nguzo kuu hatuna sababu ya kufanya kazi bila ushirikiano,’’amesisitiza na kuongeza kuwa ,

Kuna watu wapo hapa ni watendaji lakini wakikuta wananchi wanalalamika kuhusu kukosa huduma bora na wao pia wanalalamika wakati wao ni sehemu ya serikali, mnapaswa kuisemea serikali mambo mazuri na kuzingatia kutatua kero za wananchi kenye ngazi ya msingi,’’ameeleza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com