Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATAALAMU WA UBONGO NA MISHIPA YA FAMAMU KUSINI MWA JANGWA LA SAHARA WAKUTANA MLOGANZILA


Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu namna ya kubaini na kumhudumia mgonjwa mwenye changamoto za magonjwa ya Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu hapa nchini kwa kutambua kuwa magonjwa hayo yamekuwa tishio duniani.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Idara ya Matibabu nje ya nchi Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita alipokuwa akifungua Kongamano la Mafunzo ya 14 ya Mishipa ya Fahamu na Ubongo Kusini mwa Jangwa la Sahara linalofanyika kwa siku nne Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Dkt. Asha amebainisha kuwa tatizo la Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu hususani kiharusi ni kubwa ulimwenguni ambapo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kila baada ya sekunde 40 mtu mmoja hupata ugonjwa wa kiharusi na kila baada ya sekunde 3.5 mtu hufariki dunia kwa ugonjwa huo duniani.

“Magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza ni hatari sana na wataalamu wake ni wachache kwa hapa nchini tunao Madaktari Bingwa wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu wapo 14 tu ambapo kati yao, madaktari watu wazima ni 11 na kwa upande wa watoto ni watatu tu, ndio maana Serikali imeendelea kuweka msukumo wa kuwaendeleza watalaamu hususani wa mishipa ya fahamu na kuishauri jamii kufanya mazoezi na kula mlo kamili” ameongeza Dkt. Asha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Fahamu, Prof. William Matuja amesema kongamano hilo limehusisha wataalamu kutoka hospitali za hapa nchini pamoja na wataalamu kutoka zaidi ya nchi 15 Duniani ikiwemo kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Prof. Matuja ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo wataalamu hao watapata fursa ya kubadilisha ujuzi na uzoefu wa kuhudumia wagonjwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu ambapo wanaamini kuwa maarifa hayo yatasaidia kuendelea kuboresha utendaji kazi wa wataalamu katika maeneo yao ya kutolea huduma.

Naye, Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi ameishauri jamii kupima afya zao mara kwa mara kwakuwa magonjwa ya kiharusi hutokea ghafla hivyo mtu akipima afya yake mapema anaweza kujitambua na kuchukua hatua stahiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com