Na Happiness Shayo-Same
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameahidi kujenga kisima kikubwa cha maji katika Shule ya Sekondari Kibacha Wilayani Same, kwa lengo la kuendeleza kilimo cha mbogamboga na kuboresha lishe bora shuleni hapo.
Ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 katika mahafali ya 7 ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Kibacha, Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
"Nimeguswa na ujumbe wa igizo la Watoto hawa kuhusu changamoto ya maji, naomba nitamke kuwa nitaijengea shule hii Kisima kikubwa cha maji ambacho pia kitawezesha kuendeleza kilimo cha mboga mboga na viazi lishe kwa ajili ya kuchangia lishe ya watoto wetu na hivyo kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha suala la lishe shuleni linapewa kipaumbele" Mhe. Kairuki amesisitiza.
Mhe. Kairuki amefafanua kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na ilishaiona changamoto ya maji wilayani hapo hivyo, ipo kwenye hatua nzuri ya ukamilishwaji hadi kufikia mwaka 2024 Wilaya ya Same itakuwa na maji ya kutosha.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya elimu ili kuboresha sekta hiyo.
" Serikali kupitia Mradi wa Lipa kulingana na matokeo imetoa shilingi Billioni 7.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita kote nchini."
Ameongeza kuwa Serikali pia imetoa shilingi Billioni 48 kujenga Shule za Wasichana za Bweni katika mikoa 16 Tanzania Bara na kupitia Mradi wa SEQUIP.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amewaasa vijana wanaohitimu Kidato cha nne kuzingatia maadili ya Mtanzania na kuzingatia masomo.
"Vijana mnaohitimu Kidato cha Nne mwaka huu, mnapaswa kuelewa kuwa wazazi wenu na Taifa lina matarajio makubwa kutoka kwenu. Mnapaswa kuweka jitihada katika masomo yenu na kuwa na maadili mema kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu ma msijiingize katika maadili yanayofedhehesha utamaduni wetu ikiwemo ushoga na mengineyo." Mhe. Kairuki amesema.
Social Plugin