Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) tawi la Shinyanga umezindua wiki ya huduma kwa wateja katika kuhakikisha linaboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uhusiano kwa wateja.
Ufunguzi wa wiki ya huduma kwa wateja ukiongozwa na kauli mbiu ya "Ushirikiano kwa huduma bora", umefanyika leo Jumatatu Oktoba 02, 2023 katika ofisi za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga Amina Mdabi amewashukuru wateja kwa kuendeleakujiunga NSSF huku akiahidi kuwa NSSF itaendelea kutoa huduma kwa ufanisi na kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya rushwa.
Pia amewahimiza wananchi wote kwa ujumla kujiunga na mfuko ili kuweza kunufaika na mafao yanayotolewa na mfuko kwa kuwa mfuko umepanua uigo wa wanachama kutoka sekta binafsi hadi sekta isiyo rasmi.
"Niwapongeze watumishi wote kwa ujumla kwa juhudi kubwa za pamoja mnazozifanya katika kuwahudumia wateja wetu , mfuko unatambua mchango wenu katika kutekeleza majukumu mliyonayo naomba muendelee kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa ambayo ni kero na inadumaza maendeleo katika jamii",amesema Amina.
"Aidha nichukue fursa hii kwa niaba ya Mfuko kumpongeza mtoa huduma namba moja Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa zinazofanywa chini ya uongozi wake kwa kuboresha miundo mbinu madarasa katika shule zetu za umma na hospitali, ukamilishaji wa miradi ya kimkakati ambayo inachochea kuimarika kwa uchumi na maisha ya wananchi pamoja na maslahi ya wafanyakazi",ameongeza Amina.
Nao baadhi ya wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kwenye ufunguzi huo akiwemo Dorica Bushu na John Ndama wamesema wanaishukuru NSSF kwa kuendelea kuwajali kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa kupitia mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii.
Social Plugin