Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Wilaya ya Kongwa Mkoani hapa imepokea jumla ya Shilingi 238,848,519.12 kutoka Program ya "P4R" inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kuboresha miundombinu ya maji safi na usafi wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mkoani hapa Remidius Mwema ameeleza hayo kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) wakati akiwasilisha mada kuhusu mradi huo unaolenga uendelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira (P4R)na kueleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha jamii inaishi kwenye mazingira mazuri.
Amesema,Wilayani Kongwa Programu hiyo inatekelezwa katika zahanati tatu za Manyata, Hembahemba na Msunjilile ambazo zimetengewa jumla ya shilingi 160,723,614.00 huku CHMT ikitengewa Shilingi 78,124,905.12.
"Programu ya hii ya "P4R" inatekelezwa Kwa ushirikiano wa Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kupitia "force Account" katika Halmashauri 137 ndani ya mikoa 25 ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024,Mkoa wa Dodoma na Halmashauri 6 zikiwa ni miongoni mwa wanufaika katika awamu ya pili, "amefafanua
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kongwa ametumia nafasi hiyo kuwataka wasimamizi wa miradi ya kijamii wilayani humo inayotumia fedha za umma kuandaa bajeti zenye tija ili kuyafikia malengo ya miradi hiyo badala ya kuweka vipaumbele kwenye malipo ya posho na maslahi binafsi.
Mbali na hayo pia amesisitiza kuwa mapitio ya bajeti katika mradi wa "P4R" yanapaswa kutiliwa mkazo ikiwa ni pamoja na kuleta Matokeo chanya kwenye jamii huku suala la tahadhari ya mlipuko wa Surua likisimamiwa kikamilifu.
Naye Mratibu wa Chanjo na mnyororo baridi Kongwa (DIVO) Cosmas Mlimila ametoa tahadhari ya Mlipuko wa ugonjwa wa Surua, na kwamba huduma ya chanjo kwa watoto wote ambao hawakukamilisha au kutochanja kabisa inatarajiwa kutolewa kwa misingi ya dharula.
Mlimila amezitaja dalili za ugonjwa wa Surua kuwa ni pamoja na Homa kali, Vipele, Macho kuwa mekundu, Kikohozi na Mafua Huku athari zake zikiwa ni Nimonia kali Upofu wa Macho, Homa ya uti wa mgongo na hatimaye Kifo. Aidha alifafanya kuwa ugonjwa wa Surua husambazwa kwa njia ya Kikohozi au chafya kutoka kwa mtu aliyeambukizwa na dalili zake huweza kuonekana kuanzia siku 7 hadi 18.
Ameitaja mikakati ya kukabiliana na Ugonjwa wa Surua Wilayani Kongwa kuwa ni pamoja na kuwatafuta watoto wote ambao hawajakamilisha chanjo au kutochanja kabisa, utoaji wa Elimu Kwa Jamii na kurahisisha upatikanaji wa chanjo ili kuimarisha huduma za mkoba.
Kwa upande wake Afisa Afya Wilaya ya Kongwa Abdulrahman Shehe Othman ametaja malengo ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya Maji na Usafi wa Mazingira katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya katika Halmashauri, Kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika ngazi ya kaya pamoja na kuhimiza tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Social Plugin