Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROGRAMU YA KUWAJENGEA UWEZO WAFANYABIASHARA WA NDANI YA BARRICK YAWAFIKIA WAFANYABIASHARA MKOANI MARA


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, akihutubia washiriki wakati wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Programu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa ndani (Local Business Development Programme) yaliyoandaliwa na Mgodi wa Barrick North Mara na kufanyika mjini Tarime.
Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, akiongea wakati wa mafunzo ya Programu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa ndani yaliyoandaliwa na Mgodi wa Barrick North na kufanyika mjini Tarime.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda akimkabidhi Mwalimu Mwita kutoka taasisi ya Mwera Foundation kitabu chenye fursa za uwekezaji katika mkoa wa Mara.
Mmoja wa washiriki kutoka kampuni ya RIN, Isaac Range, akiongea mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Mkoa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda, katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo

****
Programu ya maendeleo ya kibiashara ya Barrick, (Local Business Development Programme) inayolenga kuimarisha uwezo wa biashara za ndani ili ziweze kunufaika na fursa zilizopo kwenye sekta ya madini imewafikia wafanyabiashara mkoani Mara kupitia mafunzo maalum ya biashara ya siku mbili yaliyofanyika mjini Tarime na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda.

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha wafanyabiashara waliopo katika sehemu ya mnyororo wa thamani hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Sky mjini Tarime, na yaliendeshwa na wataalamu kutoka kampuni ya ushauri wa masuala ya biashara na ujasiriamali ya Impacten.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo, Said Mtanda, aliipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanzisha programu ya kuwajengea wafanyabiashara uwezo na kuongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanawaongezea washiriki uelewa na yatawawezesha kuwa na vigezo vya kunufaika na fursa mbalimbali za kibiashara ndani na nje ya mgodi wa Barrick North Mara.


“Mnaoshiriki programu hii ya mafunzo muizingatie kikamilifu ili mkidhi vigezo vya kufanya kazi na mgodi huu, najua baada ya mafunzo haya mtapata fursa za kibiashara ndani na nje ya mgodi, lakini pia mtapata elimu ya kuimarisha biashara zenu,” RC Mtanda amewaambia washiriki wa mafunzo hayo.

Aliipongeza Barrick North Mara kwa kushinda Tuzo ya Mlipakodi Bora Tanzania kwa mwaka jana, lakini pia kwa kuweza kutumia dola milioni 29 kwa ajili ya wazabuni wazawa wanaofanya biashara na mgodi huo.

"Lakini pia kitaifa, kwa kipindi cha robo hii ya mwaka, Barrick imetumia dola milioni 51 zilizonufaisha kampuni mbalimbali zinazofanya kazi na kampuni hiyo kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwemo utekelezaji sera ya Uwajibikaji wa Jamii (CSR) ambapo imefanikisha miradi mbalimbali ya kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo mingi tayari imekamilika na na mingine inaendelea kutekelezwa",amesema.

Aidha, RC Mtanda alisema Kampuni ya Barrick imeipatia Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari za juu (high schools).

RC Mtanda ametumia nafasi hiyo pia kuwapatia wafanyabiashara wanaoshiriki mafunzo hayo zawadi ya vitabu 10 vyenye mwongozo wa fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa Mara.

Katika hatua nyingine, RC Mtanda amewataka wazabuni wanaofanya kazi na mgodi wa Barrick North Mara kuunga mkono juhudi za kukemea na kukomesha tatizo la makundi ya watu wanaouvamia wanaojulikana kwa jina la ‘intruders’, ili waendelee kunufaika na fursa za kibiashara kutokana na uwepo wa mgodi huo.

“Waelimisheni watu waache kuvamia mgodi, msikae kimya kwa sababu ninyi pia ni wanufaika. Mgodi ukifungwa kutokana na sababu za kiusalama hata hizi dola hazitawafikia,” alisema RC Mtanda, akitolea mfano dola za Marekani milioni 29 ambazo mgodi huo umelipa kwa wazabuni wazawa kwa mwaka huu wa 2023 pekee",amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele akizungumza kabla ya kumkaribisha RC Mtanda, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawafungulia wafanyabiashara hao milango ya kunufaika na fursa nyingi za kibiashara hata nje ya Tanzania.

Awali, Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, amesema mafunzo hayo yanahudhuriwa na wafanyabiashara wenye kampuni zikiwemo zinazofanya kazi na mgodi huo, na kwamba mpango huo ni mwendelezo wa jitahada zinazofanywa na kampuni kuwajengea wafanyabisahara wazawa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa uchumi wa madini.

“Sera ya Local Content, inatutaka kuwajengea Watanzania uwezo wa kushiriki vizuri kwenye shughuli zetu. Hivyo ili kuhakikisha kuwa wanashiriki kwenye mnyororo wa uchimbaji wa madini, tumekuja na Local Business Development Programme (Programu ya Kuendeleza Wafanyabiashara),” amesema Hermance ambaye alimwakilisha Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko.

Akiongea kwa niaba ya washiriki, Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Range, alishukuru kampuni kwa kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kuwa watayazingatia kwa kuwa ni fursa muhimu kwao.

 “Tumefurahi sana kwa ajili ya programu hii, tunategemea mgodi utatufanyia mambo mengi mazuri,” alisisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com