Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Dkt. Mwiga Mbesi akizungumza kwenye mradi wa bustani wa vijana Matongo uliobuniwa na Mgodi wa Barrick North Mara wilayani Tarime unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukuzaji Tija kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Yohana Madadi akizungumza kwenye mradi wa bustani wa vijana Matongo uliobuniwa na Mgodi wa Barrick North Mara wilayani Tarime unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Wakurugenzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, wakiwa kwenye mradi wa bustani wa vijana Matongo uliobuniwa na Mgodi wa Barrick North Mara wilayani Tarime unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Timu ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanakikundi wa mradi wa bustani wa vijana Matongo uliobuniwa na Mgodi wa Barrick North Mara wilayani Tarime unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Na Mwandishi Wetu, Mara
OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia timu ya Wakurugenzi ambayo ipo katika ziara maalum ya kikazi kwenye migodi ya Kampuni ya Twiga wametembelea mradi wa vijana wa bustani Matongo wilayani Tarime na kushauri mikakati endelevu ya kuwawezesha vijana wa vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Barrick North Mara ili kuondokana na vitendo vya uvamizi mgodini.
Akizungumza Novemba 28, 2023 baada ya kutembelea mgodi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana wa Ofisi hiyo, Dkt. Mwiga Mbesi, amepongeza mgodi huo kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujikwamua kiuchumi kwa kuwaandalia mradi huo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ina ratibu programu ya stadi za maisha kwa vijana inayolenga kuwawezeaha kutambua wana uwezo gani, kuchangamkia fursa zilizopo na zinazowazunguka, tutakaa na wadau wetu wakiwamo Barrick kuangalia namna ya kutunisha mfuko wetu wa Maendeleo ya Vijana ili kuendelea kutoa huduma kwa vijana,” amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukuzaji Tija wa Ofisi hiyo, Yohana Madadi, amesema katika ziara hiyo wameangalia masuala ya ajira, maendeleo ya vijana na utoaji huduma za kijamii zinazofanywa na mgodi huo.
Awali, Ofisa wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi huo, Praygod Mushi, amesema Mradi huo unaundwa na vikundi 10 vya vijana na hadi kufikia Mwezi Novemba mwaka huu tayari wameuza zaidi ya Sh.Milioni 150 na kati ya fedha hizo asilimia 40 imetengwa ili kuanzisha kikoba.
Kadhalika, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Matongo, Faustine Chacha na Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Masangola, wameshukuru uwapo wa mradi huo ambao umesaidia baadhi ya vijana waliokuwa wakivamia mgodini ‘Intruders’ kuachana na vitendo hivyo na kujikita kwenye kilimo hicho.