Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akijibu hoja zilizoibuliwa na Kamati za PAC, PIC na LAAC katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022 leo Novemba 4,2023 Bungeni Jijini Dodoma.
Na WAF Dodoma.
Watendaji saba wa Bohari ya Dawa (MSD) wameondolewa kazini kufuatia ukiukwaji wa sheria ya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya Tsh billion 3.4 kutoka kampuni ya Misri ya Al Andasia.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo wakati akijibu hoja zilizoibuliwa na Kamati za PAC, PIC na LAAC katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022 Bungeni Jijini Dodoma.
“Serikali imechukua hatua za kiutawala ambapo ilimuondoa Mtendaji Mkuu wa Bohari ya Dawa mwezi Aprili 2022 pamoja na Wakurugenzi wengine sita akiwemo wa Utawala, Fedha na mipango, Ununuzi, Usambazaji wa huduma za kanda, Meneja wa Sheria na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa MSD. Aidha ulifanyika ukaguzi maalum wa eneo la ununuzi na kubadilisha watumishi 24 kabla ya CAG kati ya Juni - Desemba 2022” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema utendaji wa sasa wa Bohari ya Dawa umeimarika baada ya kuongeza thamani ya bidhaa zilizosambazwa kutoka Bilioni 315 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 373 mwaka 2022/2023 ambapo thamani hii haihusishi bidhaa za miradi msonge.
“Katika robo ya mwaka kuanzia Julai - Septemba 2023 thamani ya bidhaa zilizosambazwa ni bilioni 113 ukilinganisha na bilioni 77 za Robo ya Julai - September 2022 Sawa na ongezeko la 45%” Amesema Waziri Ummy.
Akijibu kuhusu hoja ya serikali kutokulipa madeni ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya TSH bilioni 228, Waziri Ummy amesema Serikali imekubali kulipa Shilingi Bilioni 228 za NHIF ambazo ni deni la Wizara ya Mambo ya Ndani Shilingi Bilioni 45.4, Taasisi ya Mifupa (MOI) Shilingi Bilioni 18.2, NIDA sh. bilioni 17.3 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Shilingi Bilioni 129.
Waziri Ummy amesema kuwa madeni hayo yatalipwa ili kulinda uhai na uendelevu wa Mfuko. Mhe. Ummy ameyasema haya wakati akijibu hoja za ripoti ya CAG ya 2021/2022.
"Kila senti inayotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenda kwenye Sekta ya Afya tutaisimamia, na nitume salamu kwa Watendaji wote wa MSD na wengine wa Sekta ya Afya watakaofanya ubadhirifu hatutawavumilia, tutachukua hatua mara moja ili kulinda fedha za Serikali" amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka historia ya kutoa fedha Tsh. Trilioni 6.7 kwenye Sekta ya Afya jambo ambalo halijawahi kutokea huku akimpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Bw. Charles Kichele kwa kufanya kazi vizuri ya kikatiba ya kudhibiti na kukagua fedha za Watanzania.
Social Plugin