Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 17 Novemba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wadau wa uchaguzi katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika kutoa elimu ya mpiga kura.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 17 Novemba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Jaji Mwambegele amesema uboreshaji huo utafanyika kwenye Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Wadau hao wa uchaguzi wanajumuisha Viongozi wa Dini, Asasi za kiraia, Wahariri wa vyombo vya habari, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Vijana. Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya Tume kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa dhumuni la kuwajulisha kuhusu uboreshaji huo.
“Ninyi ni wadau muhimu wa uchaguzi kwa kuwa mna mchango mkubwa katika kudumisha demokrasia, upendo, amani na utulivu nchini. Kwa kuzingatia hilo, Tume imekuwa ikikutana nanyi kwa ajili ya kuwapa taarifa katika vipindi vya maandalizi ya kazi zake, kujadiliana kwa pamoja na kupokea ushauri na maoni mbalimbali kutoka kwenu lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi wa Tume,” amesema Mhe. Mwambegele.
Amewajulisha wadau hao kuwa majaribio ya uboreshaji yanafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe zitakazopangwa na kutangazwa na Tume.
Majaribio ya uboreshaji yatahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kundi lingine litakalohusika kwenye zoezi hili ni; wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.
Majaribio ya uboreshaji yatafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura. Kati ya hivyo, vituo 10 ni vya Kata ya Ng’ambo na vituo sita (6) ni kutoka Kata ya Ikoma. Vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima akiwasilisha mada katika mkutano huo.
Social Plugin