Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala akishuhudia wakati msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano Juma Gervas, akimkabidhi kadi ya mpiga kura Wilson Shango mwananchi wa Kata ya Ng'ambo Halmashauri ya Tabora mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Masempele.
Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala akipata maelezo kutoka kwa msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano Juma Gervas wakati akichukua taarifa za Wilson Shango mpiga kura wa Kata ya Ng'ambo Halmashauri ya Tabora alipokuwa akijiandikisha katika kituo cha hicho.
Afisa Tehama Mkuu Tume ya Uchaguzi NEC Bw. Lazaro Madembwe akishuhudia wakati Mwandishi Msaidizi Tume ya Uchaguzi Bw. Mwandishi Msaidizi NEC Bw. Emmanuel Madaha alipokuwa akichukua taarifa na mmoja wa wananchi waliofika kwenye kituo cha Masempele ili kujiandikisha kwenye daftari la Kudumu la Mpiga kura katika Halmashauri ya Tabora.
Gasper Kiswaga Msimamizi wa kituo cha Kizigo akiendelea kuchukua taarifa za mpiga kura Zuhura Masoud aliyefika kujiandikisha katika kituo cha Kizigo Halmashauri ya Tabora mkoani humo.
Akimu Gervas Kinyaga Mwandishi Msaidizi Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC akimuandikisha Bw. Simon Nicholas Mlimanazi katika kituo cha kujiandikisha cha Kizigo Halmashauri ya Tabora.
************
Na Mwandishi Wetu, Tabora.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema zoezi la uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la mpiga kura katika Kata za Ikoma iliyoko wilayani Rorya mkoani Mara na Kata ya Ng'ambo iliyoko Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora linaendelea vizuri, huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa watu.
Akizungumzia zoezi la uboreshaji wa majaribio ya daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha Masempele, Kata ya Ng'ambo Mkurugenzi wa Daftari na Tehama , Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Bw. Geofrey Mpangala, amesema , kuwa zoezi linaendelea vizuri na hadi kufikia Novemba 24, 2023 mwitikio wa wananchi ni mkubwa.
Amesema Kata ya Ikoma kuna vituo sita na kata ya Ng'ambo vituo kumi ambapo kwa kata ya Ikoma jumla ya wapiga kura 310 walijiandikisha na walioboresha taarifa zao walikuwa 71. Hata hivyo hakuna aliyeondolewa kwenye daftari la mpiga kura.
Ameongeza kuwa kwa Kata ya Ng'ambo jumla ya wapiga kura wapya 484 walijiandikisha, huku walioboresha taarifa zao wakiwa 309 na aliyeondolewa kwenye daftari la mpiga kura alikuwa mtu 1 tu.
Takwimu za Jumla mpaka jana kwa kata zote mbili wapiga kura wapya waliojiandikisha walikuwa 704 na walioboresha taarifa zao walikuwa 380 huku aliyeondolewa kwenye daftari alikuwa mmoja.
"Tunao mfumo wa kuboresha taarifa za wapiga kura kwa njia ya mtandao (OVRS ) Lakini mpaka sasa hakuna aliyeboresha taarifa hizo kwa njia ya mtandao. Hivyo, kuna kila sababu ya kuelimisha zaidi wananchi ili wauelewe zaidi mfumo huo wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mtandao na waweze kuutumia", Amesema Mpangala.
Naye msimamizi wa kituo cha Masempele katika Kata ya Ng'ambo , Bi. Mwatano Juma Gervas, amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri kwani wapiga kura wote wanaofika katika Kituo hicho wanafuata taratibu zote za uandikishaji kwa kutoa taarifa zao muhimu kwa ajili ya kuandikishwa au kuboresha taarifa zao.
Aidha, mpiga kura aliyefika katika Kituo cha Kizigo kwa ajili ya kujiandisha Bw. Simon Mlimanazi, amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri kwani katika kituo hicho amepata huduma kwa wakati na amekamilisha taratibu zote hatimaye amekabidhiwa kadi yake ya mpiga kura.
Ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kabla muda haujaisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura kwakuwa hili ni jambo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni ilitangaza kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023 kuanza zoezi la uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara .
Social Plugin