Wachimbaji wadogo wa eneo la uchimbaji wa madini la Sekenke,Wilaya ya Iramba Mkoani Singida leo wamepatiwa Leseni za uchimbaji na uchenjuaji wa Madini.
Zoezi la kukabidhi Leseni hizo limefanya na Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde leo katika eneo la Sekenke kufuatia maombi ya Mbunge wa Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha Mh. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba aliyoyawasilisha kwa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
Akitoa maelezo ya awali,Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba amesema eneo ambalo linatolewa leseni ni eneo ambalo lilikuwa na Leseni ya utafiti ambayo imeisha muda wake wa uhuishaji na kurejea serikali kwa mujibu wa Sheria.Jumla ya Maombi 88 ya Leseni yamepokelewa na kufanyiwa kazi katika eneo hilo ambapo ni maombi 28 tu ndio yamekidhi vigezo.
Akihutubia umma wa wachimbaji,Waziri Mavunde amesema ni maelekezo ya Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwapatia maeneo ya uchimbaji wachimbaji wadogo kwa lengo la kuongeza ushiriki wao katika sekta ya Madini na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Waziri Mavunde amewataka wachimbaji waliopewa leseni kuzitumia kwa kufanya shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia sheria na kanuni bora bila kusahau kulipa kodi na tozo ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mh. Peter J. Serukamba amesema uamuzi wa kuwapa Leseni wachimbaji hao kupitia maelekezo aliyotoa Mh Rais Dkt Samia S. Hassan yatachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Iramba na serikali itaongeza mapato yake yatokanayo na kodi na ushuru mbalimbali na hivyo kuongeza mchango wa mkoa wa Singida kwenye mapato ya serikali yatokanayo na maduhuli ambapo kwa mwaka huu wa fedha Singida imepewa lengo la kukusanya Bilioni 12 kwa mwaka na mpaka sasa wameshakusanya Bilioni 6 kabla ya robo ya pili.
Naye Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kwa niaba ya wachimbaji wa Sekenke amemshukuru sana Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kufuatia maombi ya wachimbaji hao kupatiwa leseni na kuahidi kwamba watahakikisha maeneo hayo ya uchimbaji yanakuza uchumi wa wachimbaji hao na Taifa kwa ujumla huku akiwaahidi kuwaunganisha na Taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo na mitaji ya kuendesha shughuli zao.