Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MKUDE AFUNGA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA... 224 WAHITIMU

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph M. Mkude  amefunga mafunzo ya jeshi la akiba (Mgambo) tarehe 14/11/2023, katika viwanja vya shule ya Msingi Idukilo, kata ya Idukilo  mafunzo yaliyojumisha wahitimu  224 wanawake 17   na wanaume  207.


Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ametoa pongezi na shukrani kwa viongozi wa kata ya Idukilo kwa kuhakikisha mafunzo ya  jeshi la akiba "Mgambo" yameanza na kumalizika salama, Pia amewashukuru Wakufunzi waliohusika kutoa mafunzo na kuwafanya wanafunzi kuhitimu mafunzo hayo kwa viwango vinavyohitajika.

" Ninawapongeza na kuwashukuru  sana wakufunzi wote mliotoa mafunzo haya ya viwango vinavyohitajika, wahitimu wote mkawe mstari wa mbele katika kuilinda, nchi yenu na kuwa mstari wa mbele  kujitolea kazi mbalimbali za ujenzi wa Taifa, 
Vilevile mafunzo mliyoyapata yakawe ni sehemu ya kupeleka elimu kwa jamii juu ya maadili mema, ikiwa ni pamoja na kushirikiana  na vyombo vya Ulinzi na usalama katika kutoa taarifa za uhalifu popote pale unapotokea", amesema Mkude

Aidha Mheshimiwa Mkude  ametoa wito kwa makampuni yote ya ulinzi wilayani kuajiri vijana waliopitia katika mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) na kuwapa kipaumbele katika nafasi za Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT ).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu Ndugu. Emmanuel Johnson  amewapogeza wahitimu pamoja na wakufunzi kwa kumaliza salama mafunzo pamoja na kuahidi kutenga bajeti kupitia Mapato ya ndani kwaajili ya sare za Jeshi la akiba 

Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCD) Wilaya ya  Kishapu  Bi. Esther Gesogwe Amewataka wahitimu wote kuhakikisha usalama maeneo yote ambayo watakuwepo na kushirikiana kwa ukaribu na Jeshi la Polisi  pamoja na kuimarisha amani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com