SERIKALI YATOA MWELEKEO WA UTATUZI CHANGAMOTO MIRERANI


Na.Samwel Mtuwa - Manyara.

Serikali kupitia Wizara ya Madini imesema inatambua changamoto  mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara na ina mipango ya mda mrefu na mda mfupi ya  kutatua  changamoto hizo.

Hayo yamebainishwa  Novemba 17,2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite , wafanyabiashara na wamiliki wa vitalu vya uchimbaji madini katika mkutano maalum ulioitishwa na Serikali ili kujadili changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Mapema baada ya Mkuu wa Mkoa wa  Manyara Queen Sendiga kutoa taarifa , wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya Tanzanite walielezea juu ya changamoto walizonazo ikiwa pamoja na ukosefu wa Nishati ya Umeme katika migodi , mitobozano chini ya ardhi , ubovu wa miundombinu ya Barabara, kukosekana kwa minada ya kuuza madini , ukosefu wa maji na vituo vya afya, ukosefu wa mitaji ya kuendeleza uchimbaji na vifaa duni vya uchimbaji.

Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ya kutatua changamoto hizo Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupitia upya kanuni za masoko pamoja na kuendeleza eneo tengefu la Mirerani  kwa ajili ya kuhusisha mnyororo mzima wa biashara ya Tanzanite.

Kuhusu Mitobozano , Waziri Mavunde amesema hakuna sheria inayoruhusu mitobozano katika uchimbaji madini kisheria leseni zote zina mipaka hivyo kila mchimbaji hazingatie mipaka yake iliyopo katika leseni kwa kufanya hivyo kutaondoa kero na changamoto zinazotokana na mitobozano chini ya maduara.

Akijibu hoja ya kuwepo kwa kituo cha afya katika mgodi , Waziri Mavunde ameeleza kuwa mpango wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) imepanga kuweka vituo vya afya kumi na moja katika wilaya ya Simanjiro na baadhi ya vituo vitajengwa ndani ya mgodi ili wachimbaji waweze kupata huduma ya haraka ndani ya mgodi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga  amemtaka Meneja wa TANESCO  wilaya ya Simanjiro ifikapo siku ya  jumatatu kupeleka mpango kazi wa usambazaji  umeme katika maeneo yanayohitaji huduma hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya Nishati ya  Umeme ipo katika eneo ambalo kwasasa bado hawaitaji huduma hiyo.

Akifafanua kuhusu uwezeshwaji wa mitaji na vifaa vya kufanyia kazi , Waziri Mavunde amesema tayari timu maalum imeishakaa na taasisi za fedha na Benki 42 kuangalia namna bora ya kutoa mikopo kwa wachimbaji ambapo tayari yameridhia kutoa mikopo.

Aidha, Waziri ameongeza kuwa Benki ya Maendeleo ya Biashara (CRDB) imepanga kununua mashine ya kisasa ya Uchenjuaji Madini (CIP) katika maeneo ya Nyag'hwale ,Mbogwe na Mwakitolyo kwa kuanzia.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher  Ole Sendeka ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Dkt .Samia S. Hassan kwa kuwapelekea fedha za maendeleo katika sekta ya Afya , miundombinu ya Barabara ambapo sasa kuna  mpango wa ujenzi wa vituo kumi na moja vya afya kujengwa ikiwa pamoja na ujenzi wa barabara ya kuelekea katika mgodi wa Mererani  yenye urefu kilomita zaidi tano.

Sambamba na mipango hiyo Waziri Mavunde amewataka wachimbaji kutojihusisha kwa namna yoyote ile katika  utoroshaji wa madini kwani Serikali ipo macho na haitakuwa na mjadala kwa muhusika zaidi ya kumfutia leseni.

Pia, Waziri Mavunde alipata fursa ya kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mnada wa madini ya Tanzanite lililopo eneo la  Mirerani pamoja na kutembelea sehemu za uchimbaji madini katika migodi na kuzungumza na  vikundi vinavyojihusisha na shughuli za kiuchumi ndani ya mgodi.

Ziara hii ilijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Kisiasa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Manyara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post