Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WAHITIMU CHUO CHA MISITU OLOMOTONYI KULETA MAPINDUZI KATIKA SEKTA YA MISITU NA UHIFADHI NCHINI

Na. John Bera

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wahitimu wa Chuo cha Misitu Olomotonyi (FTI) kutumia elimu waliyoipata kuleta mapinduzi katika uhifadhi misitu nchini kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na cha baadae.


Rai hiyo imetolewa Novemba 24 , 2023 na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Deusdedith Bwoyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas wakati wa mahafali ya 83 ya Chuo cha Misitu Olomotonyi (FTI) kilichopo Jijini Arusha.


“Ni vyema mkajiendeleza kielimu na kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kwa uaminifu ili kuendelea kulinda maslahi ya nchi hasa katika sekta hii ya misitu’’, amesema Bwoyo.


Amesema wahitimu wa taaluma ya misitu, usanifu wa mandhari pamoja na jioinfomatiki na usimamizi wa maliasili ni moja ya hazina ya nchi kwani taifa linahitaji wahitimu wenye ujuzi wa kutosha na nidhamu kwa ajili ya kuhifadhi na kusimamia matumizi endelevu ya misitu hapa nchini.

Aidha, Bwoyo amewataka wahitimu hao kuitenda haki sekta ya misitu pindi watakapopata fursa ya ajira huku akiwataka kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani rushwa inahujumu uhifadhi.

Sambamba na hayo, Bwoyo ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Chuo, Menejimenti na Wafanyakazi wote kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaandaa vijana wa kulinda, kuhifadhi na kuendeleza misitu nchini.


Naye Bw. Imani Nkuwi, akizungumza kwa niaba ya Dkt. Edward Kohi Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo cha Wizara alisema wizara itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu chuoni hapo kwa kukarabati miundombinu hususan majengo, kuhuisha mitaala ili iendane ma mahitaji ya sasa na pia kuanzisha programu maalum kwa ajili ya kuwakuza wajasiriamali (incubation program) ili kuwawezesha kujiajiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Misitu Olomotonyi (FTI), Dkt. Joseph Makero ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake kwa kuendelea na jitihada za kukisaidia chuo hicho kwa maslahi mapana ya uhifadhi nchini.


Katika mahafali hayo ya 83, jumla ya wahitimu ilikuwa ni 800 kutoka ngazi tofauti ikiwemo Astashahada ya Awali ya Misitu, Astashahada ya Misitu , Stashahada ya Misitu, Stashahada ya Misitu ya Mjini na Usanifu wa Mandhari, Stashada ya Jioinfomatiki pamoja na Usimamizi wa Maliasili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com