Na Mariam Kagenda - Muleba
Moto umeunguza vifaa vyote vya wanafunzi wa chuo cha Kiislamu cha Umaru Ibn Khatwabi kilichopo kata ya Muleba wilayani Muleba mkoani Kagera wakati wanafunzi hao wakiwa msikitini.
Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga amesema kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha moto huo ulioanza alfajiri ya jana kimetokana na hitilafu ya umeme katika bweni la wanafunzi wa chuo hicho.
Dkt. Nyamahanga amesema kuwa hakuna mwanafunzi yeyote aliyedhurika kwani wakati moto huo unatokea walikuwa msikitini ambapo vitu vilivyoungua ni magodoro 69 na vitanda pamoja na vifaa vyote vya wanafunzi.
Amesema kuwa mpaka sasa serikali kwa kushirikiana na mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini Dkt Oscar Ishengoma Kikoyo wamefanikiwa kutoa magodoro 69 pamoja na mablanketi 69 ambapo amewahimiza wadau wa maendeleo kuendelea kutoa msaada kwa watoto hao kwani vifaa vyao vyote vimeungua.
Naye mkuu wa chuo hicho Hassan Juma amesema kuwa chuo hicho ni cha kidini ambacho kinatoa mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa watoto wa kiume ambapo kina jumla ya wanafunzi 69 na baada ya moto huo kutokea wanafunzi wote wako salama.
Ameongeza kuwa wanafunzi hao wamehamishiwa kwenye jengo jingine kwani hata paa za bweni zimeungua hivyo linatakiwa kukarabatiwa.