Na Mariam Kagenda _ Muleba
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga amezindua rasmi mashindano ya mpira wa Miguu ya Muhalila Cup ambayo yanafanyika kata ya Kagoma wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Akizungumza wakati akizindua mashindano hayo Dkt Nyamahanga amesema kuwa michezo inajenga umoja,inaleta upendo na kufahamiana kupitia michezo hivyo anaishukuru kamati ya maandalizi ya mashindano hayo.
Dkt. Nyamahanga amesema serikali haijaiacha nyuma michezo kwani iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi hivyo wananchi wanatakiwa kushiriki kwa pamoja katika mashindano hayo.
Naye Mkurugenzi na muandaaji wa mashindano hayo Bwana Fortunatus Muhalila amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji vya vijana kupitia mchezo wa mpira ambapo mashindano hayo hufanyika mwezi Novemba kila mwaka.
Ameongeza kuwa tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2015 wapo vijana wengi ambao wameshafanikiwa kupitia mashindano ya Muhalila cup kwani yupo kijana mmoja ambaye anachezea timu ya Kagera Sugar alitokea katika mashindano hayo.
Amesema kuwa lengo lake kubwa ni kuona vijana wenzake wenye vipaji wanatoka hapo walipo wanasonga mbele na kuwapa fursa vijana kuonyesha vipaji vyao ili waweze kuonekana
Kwa upande wake mgeni maalum ambaye ni mtangazaji wa habari za michezo kutoka Cloud Tv Shafii Dauda amesema kuwa yeye kama mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Ndondo atahakikisha wanashirikiana na wadau wa michezo ili kuendeleza vipaji vya vijana kupitia michezo ili waweze kusonga mbele.
Wakati akisoma risala Bwana Omary Rwakyaya amesema kuwa jumla ya timu 16 zitashiriki mashindano hayo ambayo yatahitimishwa mwishoni mwa mwezi Desemba na Mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi milioni 2, mshindi wa pili milioni 1 na mshindi wa 3 laki 5.
Wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo Timu ya New Muleba Breaking News Fc imeifunga bao mbili timu ya Muyenje .