#Yampongeza Mama Samia kwa kuruhusu matumizi ya bando, yawahamasisha wananchi kutumia mfumo huo
Na MWANDISHI WETU
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imesema uamuzi wa kujengwa kwa Daraja la Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam ni wa kizalendo kutokana na tija kubwa inayopatikana kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Makamu Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Vuma Augustine alisema hayo tarehe 16 Novemba, 2023 wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara ya kutembelea mradi wa daraja hilo uliojengwa kwa ubia baina ya Serikali na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Nichukuie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa uamuzi nzuri wa kujenga daraja hili na pia niipongeze NSSF kwa maamuzi mazuri na wa kizalendo wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili, huu ni uamuzi nzuri kwa Mfuko kufadhili mradi ambao una tija kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Vuma.
Naye, mjumbe wa kamati hiyo, George Malima (Mpwapwa), amewapongeze NSSF kwa kubana matumizi katika mradi huo jambo linalodhihirisha kuwa Mfuko unasimamiwa vizuri na viongozi wazalendo.
“NSSF tumeona imebana matumizi sana kwenye mradi huu maana taasisi nyingi haziwezi kubana matumizi, lakini hawa wameweza maana nilikuwa napiga hesabu kwa haraka haraka wamekusanya shilingi bilioni 89 lakini wametumia asilimia 16 kitu ambacho ni kigeni hivyo ninawapongeza sana,” amesema.
Kwa upande wake, Dkt. Oscar Kikoyo (Mulemba Kusini) amewaomba wananchi wa Kigamboni na watumiaji wa daraja hilo kutumia mfumo wa kidijitali kwa kulipa kwa kutumia bando ili kupunguza msongamano.
Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kutembelea na kupata taarifa kuhusu mradi huo ambao wameridhishwa na jinsi unavyofanya kazi na huduma zinazotolewa kwa kutumia mifumo ya TEHAMA.
Amesema wajumbe wa kamati hiyo walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo alichukua uamuzi wa kuruhusu kutumika kwa tozo wakati wa kupita katika daraja hilo jambo ambalo limefurahisha wananchi hususan wa Kigamboni na watumiaji wa daraja na kwamba limeleta chachu ya kuendeleza shughuli za kiuchumi.
“Nachukua fursa hii kuwapa uhakika wanachama na Watanzania kwa ujumla kuwa NSSF iko imara, uwekezaji wake umekuwa ukikua kwa kasi kubwa hasa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na yote haya yamechangiwa na uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Mshomba ametoa wito kwa wananchi na watumiaji wa daraja kuwa waendelea kutumia mfumo wa bando ambao ni rahisi na nafuu zaidi ambapo pia ametoa rai kwa waajiri na watumishi wote wa sekta binafsi wazidi kujiandikisha kwa wingi katika Mfuko.
Social Plugin