• TGNP kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya Madai ya wanawake Ijumaa
Na Mwandishi Wetu - Malunde 1 blog
Wakizungumza wakati wa warsha zinazoendendelea kama sehemu ya Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), katika viwanja vya TGNP, Mabibo, wanaharakati hao wameitaka serikali kupitia wizara ya Sheria, kuwasilisha Bungeni sheria zote zinazohusika na chaguzi ili ziweze kuwa na mtazamo wa kijinsia sambamba na kuweka mazingira salama kwa wagombea wote hasa wanawake wenye ulemavu.
Awali akiwasilisha Ilani ya Madai ya wanawake katika Uchaguzi ya mwaka 2024/2025 iliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Uongozi, mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, amesema kwamba tayari TGNP na wadau wengine walishawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria hizo ofisi ya waziri Mkuu, Wizara ya Sheria na Katiba, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) kwahiyo wanasubiria marekebisho hayo yafanyike.
“….Tulifanya tafiti na chambuzi mbalimbali kubaini mapungufu ya kisera, kisheria na kimfumo, ambayo yanakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu kwenye nafasi za uongozi na maamuzi, tunategemea mabadiliko yakifanyika tutaondoa vikwazo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kwenye uchaguzi kama wagombea na wapiga kura…” amesema Temba na kuongeza:
“ Vilevile, Ilani hii inailenga serikali iliyoko madarakani, tukiitaka serikali, taasisi na vyombo vyote vinavyohusika na uchaguzi viwajibike kuzingatia mikataba, itifaki, matamko ya kimataifa na kikanda pamoja na misingi ya kikatiba iliyoainishwa kwenye dira ya Taifa 2025, kuchukua hatua za maksudi ili kuondoa vikwazo vinavyoendeleza ubaguzi katika ushiriki wetu katika uchaguzi kama wapiga kura, au wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za ushindani na hatimaye,kustahili kushiriki katika uongozi katika nyanja mbalimbali za jamii yetu”.
Temba ameongeza kwamba, sheria walizopendekeza zifanyiwe marekebisho ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi (CAP.343) (R.E.2015) ambayo haijakazia utekelezaji wa msingi ya usawa katika teuzi za wagombea unaofanywa na vyama vya siasa bila vigezo vya uwazi, na uzingatiaji wa msingi wa usawa uliobainishwa kwenye sheria ya vyama vya siasa. Vilevile, kwenye suala la uwakilishi wa wanawake kwa kupitia mfumo wa Viti Maalumu vilivyoingiza misingi ya ubaguzi dhidi ya wanawake walioingia bungeni kwa mfumo huu. Wizara izingatie mapendekezo kama ya maadiliko ya mfumo huu kama yalivyoingizwa kwenye Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalumu ya Oktoba 2014.
Pamoja na Sheria ya Gharama za Uchaguzi (CAP 288 (R.E 2015) inayowabebesha wagombea wote mzigo wa gharama, bila kujali tofauti za kiuchumi kati ya wanawake na wanaume.
Amesema kwamba, sheria nyingine ni Sheria ya Vyama Vya Siasa (CAP 258 (RE 2015. Licha ya sheria husika kubainisha msingi wa usawa wa kijinsia kama nguzo ya kuimarisha demokrasia, sheria haijabainisha uwajibikaji wa vyama vya siasa katika kutekeleza msingi huu katika uongozi wa vyama husika na wa uteuzi wa wagombea
Ilani hii madai ya wanawake katika uchaguzi ni ya sita (6) iliyobeba madai rasmi tukiwa wadau na washiriki wakuu katika michakato mbalimbali ya uchaguzi. Ilani ya kwanza ilikuwa ya mwaka 2000 ikijulikana kama Ilani ya Wapigakura, ya pili ni ya mwaka 2005, ya tatu ni ya mwaka 2010, ya nne ni ya mwaka 2015 ya tano ni ya mwaka 2020. Maandalizi ya ilani zote sita yaliongozwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia Mtandao wa Wanawake na Katiba, Uchaguzi na Uongozi unaoratibiwa na Mfuko wa Ufadhili wa Wanawake Tanzania (WFT_T)
Social Plugin